2015-10-29 14:57:00

Baba Mtakatifu Francisko aipongeza Radio Maria kwa Uinjilishaji wenye mvuto!


Radio Maria imekuwa ni mdau muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, inaleta mvuto na mashiko masikioni na mioyoni mwa watu kiasi cha kuvutika kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Radio Maria. Ni radio ambayo imekuwa karibu sana na wasikilizaji wake, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu na hatimaye kuwapatia maneno ya faraja na matumaini.

Hii ni dhamana inayotekelezwa na Radio Maria kwa kujiaminisha katika huruma, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, Radio Maria hadi sasa haijatindikiwa mambo msingi katika kukuza na kudumisha utume wa Radio Maria nchini Italia na baadaye sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Radio Maria imepata mafanikio makubwa sana kiasi cha kuwashangaza wengi, changamoto kwa sasa ni kuendelea kuwa makini kwa kuambata teknolojia inayokwenda na wakati, ili Radio Maria iendelee kutekeleza dhamana yake.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na wajumbe pamoja na viongozi wa Radio Maria mjini Vatican, Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015. Radio Maria imefanikiwa kufikisha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu kutoka katika tamaduni, lugha na mapokeo mbali mbali, kielelezo cha ujasiri na uwazi wa kuwashirikisha na kuwamegea wengine utambulisho wa Kikristo na kupokelewa na wengine kwa moyo wa shukrani hata kama ni kwa mara ya kwanza wanabahatika kukutana na ujumbe wa Injili. Huu ni utume unaowezeshwa kwa tunza na ulinzi wa Bikira Maria, katika hali ya unyenyekevu kugeuza yale madogo kuwa makubwa, kwani ni Mama na Msimamizi wa Radio Maria.

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa Radio Maria kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa waaminifu kwa Injili, Mafundisho ya Kanisa pamoja na kusikiliza kilio cha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kuwa na mahali pa rejea na msaada katika shida na mahangaiko yao. Ni changamoto ya kutangaza Injili na Ibada kwa Bikira Maria; mambo muhimu katika kukoleza upendo wa watu kwa Kanisa na moyo wa Ibada na Sala. Hapa panakuwa ni mahali pa kusikiliza kwa makini, kujifunza kusali na kupata ufafanuzi wa mafundisho ya imani yanayojenga na kupanua wigo wa uelewa wake.

Kwa njia hii anakaza kusema Baba Mtakatifu, Radio Maria licha ya kutekeleza dhamana ya: kuhabarisha, kuburudisha na kufundisha, lakini pia inakua ni chombo cha matumaini yanayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, anayewasindikiza watu wengi katika mahitaji yao. Wajumbe hawa wamekuwa wakishiriki katika kongamano la kimataifa lililokuwa linapembua kwa kina mapana karama ya Radio Maria inayosikilizwa kila siku na zaidi ya watu millioni thelathini, mchango mkubwa unaotolewa na wapenzi wa Radio Maria sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ni huduma inayopongezwa sana na Makanisa mahalia na Jamii ya watu. Ni Radio inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa sala na shuhuda zinazowasaidia watu wengi kufungua malango yao kwa Kristo Yesu, kwa kufuata mfano wa Bikira Maria, anayepaswa kupendwa sanjari na kuzingatia Mafundisho ya Kanisa. Wadau wa Radio Maria hawana budi kukuza na kudumisha ndani mwao moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kujisomea vitabu vitakavyowawezesha kurutubisha imani yao tayari kuwa kweli ni mashuhuda wa kile wanachohubiri na kukitangaza.

Radio Maria ni chombo ambacho kinatoa matumaini ya Kikristo yanayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo Mfufuka anayeshuhudiwa kwa njia ya imani na matendo ya huruma. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka wadau wote na mipango ya Radio Maria chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na kuwapatia baraka yake ya kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.