2015-10-27 15:30:00

Zaidi ya watu 350 wamefariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi huko Pakistan na Afghanstan na kusababisha zaidi ya watu 350 kupoteza maisha na wengine wengi bado hawajulikani waliko. Katika ujumbe uliondikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Galeb Bader, Balozi wa Vatican nchini Pakistan, Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wote walioguswa na maafa haya.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikisha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Anapenda kuwafariji wote wanaoomboleza kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na majirani zao. Kwa namna ya pekee, anawahimiza viongozi wa Serikali na vikundi vya uokoaji kutekeleza dhamana hii kwa unyofu na moyo mkuu. Wote hawa anapenda kuwapatia baraka yake ya kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.