2015-10-27 14:46:00

Watanzania onesheni ukomavu wa kisiasa!


Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania inaendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba 2015 kwa amani na utulivu katika maeneo mengi ya Tanzania. Taarifa zinazonesha kwamba, kuna “vigogo” wanaoendelea kuangushwa kwenye majimbo yao na baadhi ya watu kujitangazia ushindi kinyume cha taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi mkuu nchini Tanzania, hali ambayo inaweza kusababisha mtafaruku ndani ya jamii.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anawataka watanzania wote kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi mkuu. Wagombea uongozi waoneshe ukomavu kwa kukubali matokeo na kuendelea kushirikiana kwa ajili ya kuwahudumia watanzania katika ujumla wao! Kuanguka katika uchaguzi mkuu isiwe ni sababu ya kutowahudumia watanzania!

Askofu Ngalalekumtwa anawahimiza watanzania kuvuta subira, kupokea matokeo kwa maridhiano, amani na utulivu na pale ambapo watu hawajaridhika na matokeo au jinsi ambavyo uchaguzi umeendeshwa wanapaswa kufuata sheria, taratibu na kanuni, ili haki iweze kushika mkondo wake. Vurugu na kinzani ni mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watanzania. Watanzania wadumishe amani, ili waendelee kucharuka katika demokrasia, ustawi na maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.