2015-10-27 08:45:00

Tamko la viongozi wa Kanisa kuhusu Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi, Cop21


Viongozi wa Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakiwa wamehamasishwa na Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, “Laudato si”, wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa katika mkutano wake kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Cop21, utakapofanyika mjini Paris, Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 11 Desemba 2015 kuhakikisha kwamba, wanafikia makubaliano yanayowawajibisha katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Viongozi wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia usawa unaojikita katika misingi ya sheria inayotekelezeka ili kuleta mabadiliko ya kweli! Viongozi hawa wa Kanisa wameandika ombi hili kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa niaba ya watu wanaowaongoza katika Makanisa yao, ili mkutano wa Paris, uweze kuleta matunda yanayokusudiwa kwa kuzingatia mambo makuu kumi yaliyoorodheshwa ili yaweze kufanyiwa kazi na wajumbe wakati wa mkutano wao. Haya ni mambo ambayo yameibuliwa kutokana na uzoefu na mang’amuzi ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia; watu ambao wameguswa na kutikiswa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kimsingi wanakubaliana kwamba, mazingira ni nyumba na urithi wa wote na kwamba; matunda yake yanapaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Sera na mikakati endelevu haina budi kuwahusisha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, dhana inayohitaji viongozi wajasiri watakaoweza kusimama kidete kuhakikisha kwamba, mkataba kuhusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi unawajibisha.

Viongozi wa Kanisa wanaendelea kukazia umuhimu wa kanuni maadili katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi badala ya kujielekeza kwenye sera na mikakati ya kisiasa peke yake. Ni jambo la msingi ikiwa kama wajumbe wote watakubaliana kwamba mazingira na tabianchi ni kwa ajili ya mafao ya wote na kila mtu anaguswa kwa namna yake. Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na makubaliano yanayojikita katika misingi ya usawa itakayokuwa kweli ni chachu ya mageuzi pamoja na kujikita katika uelewa wa dunia, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Viongozi wa Kanisa wanaendelea kuhimiza kwamba, kuna haja ya kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani pamoja na kuweka malengo ya kupunguza hewa ya ukaa ifikapo nusu ya Karne hii. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Visiwa vinakuwa katika hali ya usalama dhidi ya ongezeko la kina cha bahari kutokana na kupanda kwa joto, hali inayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Sheria iwekwe ili kila taifa liweze kuitekeleza kwa ajili ya mafao ya wengi. Ni wajibu wa Serikali husika kuhakikisha kwamba, zinafanya tathmini ya mara kwa mara, ili kufikia malengo yatakayowekwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Viongozi wa Kanisa wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mifumo na mitindo mipya ya maisha, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kujikita katika: usawa na mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato. Mkakati huu usaidie kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kutoka katika vyombo vya usafiri, matumizi ya kijeshi pamoja na matumizi ya nyumbani. Watu wapate huduma ya maji safi na salama; chakula bora kinachozalishwa kwa kuzingatia mbinu bora za kilimo badala ya watu kutafuta faida kubwa hali inayogumisha maisha ya watu wengi kutokana na bei kubwa ya mazao ya chakula.

Viongozi wa Kanisa wanaendelea kuhimiza kuhusu ushirikishwaji wa watu katika kupanga na kutekeleza maamuzi yatakayofikiwa na kwamba, mktaba wa Mwaka 2015 ujikite katika uhalisia wa maisha ya wananchi wengi, hususan maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ya Kimataifa ioneshe mshikamano wa upendo unaojikita katika kanuni auni, kwa kushirikishana teknolojia, ujuzi na maarifa ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwishoni, viongozi wa Kanisa katika ombi lao kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mkutano wake juu ya mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika huko Paris, Ufaransa, wanaitaka kuwa na dira pamoja na mwongozo kamili utakaofuatwa katika utekelezaji wa maazimio yatakayokuwa yamefikiwa. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanakumbushwa kwamba, mazingira ni nyumba ya wote, kumbe, wanaowajibu wa kusikiliza kilio cha maskini; waoneshe mshikamano unaojikita katika ujasiri; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi pamoja na kutunza mazingira, nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.