2015-10-27 10:24:00

Jubilei ya miaka 50 ya Waraka wa Majadiliano ya kidini!


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu  Nyakati Zetu “Nostra Aetate” unaokazia pamoja na mambo mengine majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha umoja, udugu, amani na maridhiano, kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni watoto wa Mungu na kamwe tofauti zao zisiwe ni sababu ya vita na kinzani za kidini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, kwa kutambua umuhimu wa Waraka huu katika maridhiano ya watu, haki na amani, limewaandikia Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo ujumbe wa matumaini yanayosimikwa katika umoja wa kitaifa licha ya tofauti zao za kiimani na kidini. Maaskofu wanawaalika wananchi wa Poland kudumisha majadiliano, umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Wakristo wakuze majadiliano ya kidini hasa na Wayahudi pamoja na Waislam, ili amani iweze kutawala.

Maaskofu wanasema kwamba, kwa mwamini anayebahatika kukutana na Yesu kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II anakutana pia na dini ya Kiyahudi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Wakristo na Wayahudi wanachangia pamoja amana ya maisha ya imani. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wa dini hizi mbili wanajenga na kudumisha dhamiri nyofu katika haki, ukweli na uwazi, ili kusafisha kumbu kumbu potofu zilizogubikwa na madhulumu pamoja na nyanyaso dhidi ya Waamini wa dini ya Kiyahudi.

Kuungama dhambi ya nyanyaso na dhuluma za kidini dhidi ya Wayahudi ni hatua kubwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kuendelea kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo. Dhuluma na mauaji yaliyosababishwa na utawala wa Kinazi nchini Poland pamoja na madhulumu ya Shoah; ni matukio yaliyoacha kurasa chungu katika maisha ya wananchi wengi wa Poland. Maaskofu wanamshukuru Mungu kwamba, leo hii kuna Jumuiya za waamini wa dini ya Kiyahudi wanaoendelea kuongezeka siku hadi siku, mwaliko wa kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kushirikishana amana ya maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote!

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.