2015-10-27 09:43:00

Atunukiwa Udaktari wa heshima katika utamaduni wa umoja!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, tarehe 26 Oktoba 2015 ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa heshima katika utamaduni wa umoja na Chuo kikuu cha Sophia kilichoko Loppiano, Firenze, nchini Italia. Ni kiongozi ambaye amejipambanua katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, akasimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani, ili kukuza na kudumisha umoja na udugu.

Ni kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza ameendeleza kwa ari na moyo mkuu mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika medani mbali mbali za maisha, amemtumia ujumbe Kardinali Giuseppe Betori, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Firenze, ili kumhakikishia Patriaki Bartolomeo wa kwanza uwepo wake wa karibu kwa njia ya kiroho. Anatambua mchango wake katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa umoja unaojikita katika majadiliano ya kiekumene, sadaka na udumifu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Chuo kikuu cha “Sophia” kitaendeleza karama ya umoja kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu, ili mahali hapa paweze kuwa ni kituo cha watu kukutana  pamoja na kutoa nafasi kwa tamaduni na dini mbali mbali kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.