2015-10-26 15:17:00

Vita ni chanzo kikuu cha majanga na uharibifu wa mazingira! Wala haina maana!


Wahudumu wa maisha ya kiroho katika vikosi vya ulinzi na usalama wanakabiliana na changamoto mbali mbali katika medani za kimataifa, hususan kuhusiana na dhamana ya kulinda na kudumisha: utu na heshima ya binadamu katika maeneo mapya ya vita. Hii ni hali halisi inayojionesha katika baadhi ya Nchi za Kiafrika, Ulaya na huko Mashariki ya Kati.  Haya ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2015 alipokutana na kuzungumza na washiriki ya kozi ya nne ya malezi kwa wahudumu wa maisha ya kiroho katika vikosi vya ulinzi na usalama.

Kozi hii inapania pamoja na mambo mengine, kuzuia uvunjaji wa haki msingi za kimataifa kiutu; kupunguza shida na mateso yanayosababishwa na madhara ya vita. Hii inatokana na ukweli kwamba, vita ni hali inayosambaratisha mahusiano na mafungamano wa kijamii kati ya ndugu na kati ya taifa na taifa; athari zake zinawatendea hata wale wanaojikita katika vita. Askari wengi wanaotoka mstari wa mbele wanateseka sana kutokana na madhara ya vita kwa kuonesha madonda ya ndani, kiasi kwamba, baadhi ya madonda haya yanaacha alama ya kudumu kwa wahusika.

Kumbe, ni jambo la msingi kuhakikisha kwamba, askari wanapata tiba muafaka ya maisha yao ya kiroho, msaada unaoweza kutolewa na Mama Kanisa, kwa kuonesha ule upendo wa kimama unaojikita katika mikakati bora ya kichungaji: Wahudumu wa maisha ya kiroho wawasindikize na kuwaenzi askari katika mchakato wa maisha yao, kwa kuonesha ule upendo wa kidugu unaofariji. Wanaalikwa kuwaganga na kuwaponya askari hawa kwa mafuta ya Neno la Mungu linaloponya na kuwakirimia watu matumaini; wasaidiwe kupata neema inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho; zinaorutubisha na kupyaisha mioyo iliyovunjika na kupondeka!

Utu wa binadamu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee wakati wa vita na kinzani za kijamii; kwa kuwalinda wale ambao kwa namna yeyote ile hawahusiki na vita hiyo kama wahudumu wa afya, watawa, majeruhi na wafungwa wa kivita. Lakini ikumbukwe kwamba, vita kimsingi havina maana, kwani vimekuwa ni chanzo kikubwa cha maafa, uharibifu wa mazingira pamoja na tamaduni za watu. Wadau mbali mbali hawana budi kuhakikisha kwamba, utu wa binadamu unadumishwa na wote ili kukabiliana na madhara ya vita ambayo kwa sasa ni makubwa kupita kiasi.

Mama Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema anakaza kusema, vita haina umuhimu wowote ule kwa binadamu na inapaswa kupigwa rufuku. Watu wajitahidi kujenga madaraja yanayounganisha badala ya kuta zinazowatenganisha watu; watu wajenge utamaduni wa haki, amani na upatanisho badala ya kukimbilia mtutu wa bunduki ambao umekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa binadamu; daima ikumbukwe kwamba, kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote na kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu hata wakati wa vita!

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana katika vita kuu ya tatu ya dunia, wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kusaidia mchakato wa majiundo makini: kiroho na kimaadili, ili kuwasaidia wanajeshi hao kukabiliana na magumu ya maisha, wakati wanapotoa huduma kwa nchi zao na kwa binadamu wengine. Wajengewe uwezo wa kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu kimataifa, ili kuondokana na mateso yasiyokuwa na msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.