2015-10-26 14:39:00

Kardinali Roger Etchegaray avunjika mguu na kulazwa Gemelli


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya familia, alikwenda kumtembelea Kardinali Roger Etchegaray, aliyelazwa kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma kutokana na kuvunjika kwa mguu wakati alipokuwa kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili asubuhi. Kardinali Etchegaray wakati akisalimiana na Baba Mtakatifu aliteleza na kuanguka na hatimaye, kuvunjika mguu ambao kwa sasa atapaswa kufanyiwa opresheni kubwa.

Baba Mtakatifu aliweza kuongea na Kardinali Etchegaray kwa kitambo kirefu na baadaye akampatia baraka zake za kitume na kurejea tena mjini Vatican. Kardinali Roger Etchegaray kwa upande wake, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuitisha na kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo”. Sinodi imehitimsihwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliyelitaka Kanisa kumwilisha katika maisha na utume wake Injili ya familia pamoja na kujikita katika huruma ya Mungu inayowakumbatia wote pasi na ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.