2015-10-26 09:26:00

Dumisheni haki, amani na utulivu wakati wa kusubiria matokeo ya uchaguzi mkuu


Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi zinazonesha kwamba, watanzania millioni 22.75% walijiandikisha kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika, Jumapili tarehe 25 Oktoba 2015 na kwamba, kwa sasa matokeo ya awali yanaendelea kutolewa sehemu mbali mbali za Tanzania. Huu ni uchaguzi ambao umekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa watanzania, pengine kuliko hata miaka mingine iliyopita. Kampeni zimefanywa kwa mbwembwe na majigambo makubwa, kila mgombea akinadi sera za chama chake.

Kimsingi watanzania wengi wanasubiri kuona kwamba, viongozi waliochaguliwa wanakuwa ni chachu ya mabadiliko na maendeleo endelevu kwa watanzania wengi; kwa kujikita katika: uadilifu, ukweli, uchapakazi na uzalendo; tayari kusimamia haki msingi za binadamu, maisha, amani na umoja wa kitaifa. Wasimame kidete kupambana na rushwa, umaskini, magonjwa na ujinga; mambo ambayo yanayo kwamisha maendeleo ya watanzania wengi.

Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda, ambaye amekuwa akishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia kuanzia tarehe 4 Oktoba hadi tarehe 25 Oktoba 2015, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anawasihi watanzania wakati huu wanapoendelea kupokea matokeo ya awali, kuendelea kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na mafungamano ya kijamii, huku wakivuta subira.

Ni matumaini ya Askofu Nkwande kwamba, zoezi hili limefanywa kwa uadilifu na umakini mkubwa, huku watanzania wakijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwapatia kiongozi anayefaa kwa wakati huu. Kumbe, kiongozi atakayechaguliwa na wengi apokelewe kwa shangwe na kupewa ushirikiano na watanzania wote, tayari kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya watanzania wengi. Ni kipindi cha kuvunja mitandao na makundi yaliyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi, ili kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Kwa wale ambao matokeo yatakwenda kombo, kinyume na matarajio yao, wavute subira pamoja na kuhakikisha kwamba, wanafuata mkondo wa sheria, ili kweli haki iweze kutendeka na watanzania waendelee kufurahia amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Kujichukulia sheria mkononiĀ  ni hatari kwa mustakabali wa Tanzania katika ujumla wake. Viongozi wa kisiasa wawe mstari wa mbele kudumisha amani, utulivu na haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.