2015-10-25 15:06:00

Sinodi imekuwa ni fursa ya kushuhudia na kutangaza ukuu na utakatifu wa familia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni, tarehe 24 Oktoba 2015 katika mkutano wa kumi na nane, amehitimisha rasmi vikao vya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, kwa kuwashukuru Mababa wa Sinodi pamoja na wahusika wakuu waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho haya ambayo yametekelezwa katika kipindi cha miaka miwili, kwa kuonesha ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawashukuru wote waliotekeleza dhamana hii katika hali ya ukimya, huku wakiendelea kuchangia utekelezaji wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, wote hawa wawe na uhakika kwamba, wananafasi ya pekee katika moyo wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya sala. Lakini, jambo la kujiuliza ni umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya maaskofu kuhusu familia kwa kuzingatia mwanga wa Injili, Mapokeo pamoja na historia ya Kanisa kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita.

Hili limekuwa ni tukio la kuionjesha familia ya Mungu mwanga wa imani, matumaini na furaha hata katika matatizo na changamoto zinazoendelea kuiandama na kutishia familia; katika misingi ya ukweli, uwazi na ujasiri bila kuogopa! Lengo msingi ni kutangaza na kushuhudia ukuu, uzuri na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa na familia; ndoa inayojikita katika mahusiano thabiti na huru kati ya bwana na bibi kama msingi wa maisha ya kijamii.

Maadhimisho ya Sinodi imekuwa ni fursa ya kusikiliza kilio cha familia nyingi duniani, katika shida na mahangaiko yao; katika imani na matumaini, ili kusimama kidete, tayari kushuhudia Injili ya familia, chachu ya maisha mapya na kamwe si jiwe la kinzani na shutuma dhidi ya wengine. Imekuwa ni fursa ya kufungua mioyo ya watu ambao wakati mwingine inajificha nyuma ya pazia la Mafundisho ya Kanisa kwa kuwa na moyo mgumu na kusahau kwamba, Kanisa ni la maskini na wadhambi wanaotafuta kuonja huruma na upendo wa Mungu na wala si kwa ajili ya wenye haki, watakatifu na wateule peke yao!

Sinodi imekuwa ni kipindi cha neema cha kuonesha, kulinda na kutetea uhuru wa watoto wa Mungu; kueneza uzuri wa maisha ya Kikristo kwa kutumia lugha inayoeleweka na wengi. Ni kielelezo cha umoja katika utofauti unaofumbata na kuambata umoja wa Kanisa katika majadiliano ya kweli ili kulainisha mioyo ya watu kwa kuchota utajiri wake kutoka kwa Mama Kanisa. Mababa wa Sinodi pamoja na kutambua kwa uhakika Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini pia wameonesha kile ambacho kwa wengi kimeonekana kuwa ni kashfa kwa Kanisa kwa vile tu, Mababa wa Sinodi wameonesha uhuru wa dhamiri nyofu na kwa wengine hali hii imeonekana kuwa ni jambo la watu kuchanganyikiwa!

Tofauti hizi zinajikita katika tamaduni na mahali wanapotoka watu, changamoto ni kuhakikisha kwamba, mchakato wa Utamadunisho unakuzwa na kudumishwa, ili Injili iweze kuota mizizi katika tamaduni za watu. Utamadunisho unaonesha nguvu na ukweli wa Injili. Licha ya tofauti zilizojionesha, lakini wote wanaunganishwa kwa pamoja kutambua changamoto ya sasa ni kuhubiri Injili kwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya familia dhidi ya mashambulizi, bila kuwashutumu wengine wala kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Kanisa limejitahidi kuonesha kwa ujasiri wema na huruma ya Mungu inayopita uelewa wa kibinadamu; huruma inayopania kwamba, kila mtu aweze kukombolewa. Hii ndiyo changamoto endelevu inayotakiwa kumwilishwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.