2015-10-25 14:39:00

Mama Kanisa ataendelea kutembea na familia zinazoteseka duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 25 Oktoba 2015 amehitimisha rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia kwa Ibada ya Misa Takatifu na baadaye akapata nafasi ya kusali pamoja na waamini Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uliokuwa umefurika kwa bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofika kumshukuru Mungu kwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ambayo yamedumu kwa takribani majuma matatu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi yamekuwa ni kipindi kilichojikita katika sala na tafakari kwa kuambata umoja wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamekabiliana na changamoto nzito, lakini maadhimisho haya yamekuwa kweli ni zawadi ya Mungu itakayozaa matunda kwa wakati wake. Sinodi maana yake ni kutembea kwa pamoja kwa kuonesha uzoefu wa Kanisa linalotembea kwa pamoja likiwa limeshikamana na familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Lengo anasema Baba Mtakatifu ni kuonja huruma, upendo na ubaba wa Mungu anayewajali watu wake na yuko tayari kuwaganga na kuwaponya madhaifu yao. Mwenyezi Mungu anataka kufanya Sinodi na watu wake, ili kuunda watu atakaowaongoza katika njia ya uhuru na amani, kielelezo cha familia ya binadamu inayotembea kwa kuthamini zawadi ya maisha ili kuambata baraka ya Mungu. Hii ni familia ya Mungu isiyobagua maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; familia zinazotaabikiana na kusumbukiana kwa kuiga mfano wa Kristo Bwana na Mwalimu, aliyejimwilisha, akajifanya maskini na mdogo kuliko wote, ili hata wakubwa na matajiri wa dunia hii, waweze pia kupata uzima wa milele.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, taswira ya watu wanaotembea ili kusalimisha maisha yao, imejikita katika akili na moyo wake, anapoona makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji wakiwa njiani kutafuta hifadhi Barani Ulaya. Hii ni changamoto ya watu wa nyakati hizi, lakini iko siku Mwenyezi Mungu ataweza kuwafuta machozi kwa njia ya faraja yake.

Familia za wakimbizi na wahamiaji zimebebwa pia na Mababa wa Sinodi katika sala, tafakari na ushuhuda uliotolewa na baadhi ya Mababa wa Sinodi wanaotoka katika maeneo haya. Ni watu wanaotafuta usalama na utu wao kama binadamu; wanataka kuona mwanga wa amani na kwamba, Kanisa litaendelea kuwakumbatia, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakomboa kutoka katika utuma na kuwaongoza katika uhuru kamili. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini ya kipindi cha Mwaka, inaonesha taswira ya familia ya Mungu inayotembea pamoja kielelezo cha mang’amuzi na uzoefu uliooneshwa na Mababa wa Sinodi katika kipindi cha majuma matatu ya sala na tafakari. Anamwomba Bikira Maria kwa sala na tunza yake ya kimama aliwezeshe Kanisa kudumisha ari na moyo wa umoja na udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.