2015-10-25 15:23:00

Kanisa linajali na kuheshimu utu wa binadamu wote!


Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 26 Septemba 1965, miaka hamsini iliyopita, alikutana na kuzungumza na kundi kubwa la kimataifa la Wazingari, huko Pomezia, Italia. Kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei hii ya miaka hamsini, Kanisa bado linapenda kuonesha kwamba, linawajali na kuwathamini Wazingari licha ya shida na magumu wanayokabiliana nayo, watapata tena fursa, Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2015 kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, ambalo limeandaa mkutano huu, katika Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya thelathini ya Kipindi cha mwaka B wa Kanisa, iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya “Divino Amore”, Jimbo kuu la Roma, amewahakikishia Wazingari hawa kwamba, Kanisa linawapenda, linawathamini na kutaka kuwaendeleza, changamoto ambayo ilitolewa na Papa Paulo VI, yapata miaka hamsini iliyopita.

Mahujaji hawa wameadhimisha Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, ili kukumbuka madhulumu ya watu wa “Parajmos” pamoja na kumshukuru Mungu kwa Ibada ya Misa Takatifu kwa wema, ukarimu na tunza yake ya kibaba katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Kardinali Vegliò anakiri kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu amewatendea matendo makubwa na amewaneemesha kwa vijito vya furaha na faraja. Yesu anaendelea kukutana na kuwaimarisha katika hija ya maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili waweze nao kupenda na kujenga umoja na mshikamano kati ya watu wa mataifa.

Yesu anataka kuwakirimia tena jicho la imani kama alivyofanya kwa Bartimayo kipofu anayesimuliwa kwenye Injili, tayari kuambata neema na huruma ya Mungu ili kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kumfuasa Yesu katika maisha na utume wake; kwa kuwa na uwezo wa kutambua wema na ubaya, ili kuvuka kinzani na vikwazo katika mahusiano na mafungamano ya kijamii yanayosababisha chuki, uhasama na hata mauaji ya kimbari. Hija ya mahujaji hawa anasema Kardinali Vegliò iwajalie maisha mapya, huku wakiwa wameokolewa na mwanga wa imani, tayari kuwashirikisha jirani zao imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.