2015-10-24 15:30:00

Tamko la Mababa wa Sinodi kuhusu Mashariki ya Kati, Afrika na Ukraine!


Mababa wa Sinodi wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wajumbe wote waliobahatika kushiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inayoongozwa na kauli mbiu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo, katika tamko lao la pamoja, wanapenda kuyaelekeza macho yao kwa familia zinazoendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na dhuluma huko Mashariki ya Kati, Afrika na Ukraine. Hawa ni watu wanaoteseka, lakini katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni hali yao inazidi kuwa mbaya zaidi.

Kuna mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, watu wanaonyongwa kwa sababu mbali mbali; kuna wale wanaotekwa nyara; wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu, viungo na utumwa mamboleo. Kuna waamini wanaodhulumiwa kutokana na dini, makabila au siasa. Mashambulizi haya yamekuwa pia ni chanzo cha uharibifu mkubwa wa urithi wa dunia na makumbusho ya kale pamoja na kusababisha makundi makubwa ya watu kukimbia maeneo na nchi zao, huku wakikabiliana na kifo uso kwa uso.

Ni watu ambao hawawezi tena kurudi katika maeneo yao kwani utu, heshima, haki na usalama wao umetiwa rehani, lakini wakipewa fursa, wanaweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Mababa wa Sinodi wanaendelea kukazia umuhimu wa Familia ya Mungu katika ujumla wake kuishi kwa kuzingatia: haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu; zawadi ya uhai, uhuru wa kidini na haki za kimataifa. Wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na Familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, ikumbuke kwamba, kuna watu wanawaombea na kuwasindikiza katika shida na mahangaiko.

Mababa wa Sinodi wanatambua na kuwaombea watu waliotekwa nyara au kupotea katika mazingira tatanishi, waweze kuachiliwa huru pamoja na kuunganisha sautiili kupinga vita, kinzani, vitendo vya kigaidi, dhuluma, nyanyaso na uharibifu wa rasilimali na urithi wa dunia. Mababa wa Sinodi wanataka vita na chuki kukoma mara moja pamoja na kudhibiti biashara ya silaha ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa binadamu. Amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati iwe ni matunda ya sera nzuri za kisiasa zinazoheshimu tamaduni, dini na mataifaya watu.

Mababa wa Sinodi wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa nchi ambazo zimeendelea kuwa mstari wa mbele kuwahudumia pamoja na kutoa hifadhi kwa wahamiaji na wakimbizi. Wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya migogoro hii kwa njia ya diplomasia na haki msingi za kimataifa sanjari na majadiliano, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu tofauti za kiimani zisiwe ni chanzo cha vurugu, bali chachu ya mshikamano katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani.

Amani inaweza kupatikana sehemu mbali mbali za dunia ambako bado mtutu wa bunduki unarindima, ikiwa kama watu wanajikita kwa mara nyingine tena katika mchakato wa upatanisho ambao ni matunda ya udugu, haki, heshima na msamaha. Ni hamu ya Mababa wa Sinodi kwamba, amani iweze kutawala katika akili na mioyo ya watu. Kiu ya amani na utulivu iziendee pia familia zinazoishi katika mazingira magumu Barani Afrika, huko Mashariki ya kati na Ukraine. Mababa wa Sinodi wanahitimisha tamko lao kwa kuziweka familia zote chini ya ulinzi na tunza ya familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.