2015-10-24 09:32:00

Silaha za nyuklia bado ni tishio kwa amani na usalama wa dunia!


Maendeleo na hatimaye usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia  ni mambo ambayo yako kinyume kabisa cha moyo na tunu msingi za Umoja wa Mataifa. Kutokana na mwelekeo huu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, Mkataba wa udhibiti wa utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia unatekelezwa pamoja na kupiga rufuku utengenezaji wa mabomu ya atomic. Huu ni mchango ambao umetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa.

Vatican kwa mara nyingine tena inapenda kukazia kwamba, utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za kinyuklia ni jambo linalohatarisha amani na utulivu na kwamba, ni mambo yanayokwenda kinyume kabisa cha udugu na kanuni maadili. Askofu mkuu Auza anapongeza hatua ambazo zimefikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika udhibiti wa nguvu za nyuklia nchini Iran, katika mkataba uliotiwa sahihi hivi karibuni huko Vienna.

Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba kinzani na migogoro iliyokuwa inasababishwa na uwepo wa silaha za kinyuklia nchini Irani, pole pole itaanza kutoweka na watu kuwa na amani na utulivu wa ndani. Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaotaka kudhibiti utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia ni muhimu sana katika mchakato wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kujenga, kudumisha na kuimarisha amani na utulivu; mambo msingi katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu. Bila kuzingatia mambo haya, ajenda ya Maendeleo kimataifa ifikapo mwaka 2030, iliyozinduliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, itakuwa ni ndoto ya mchana anasema Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.