2015-10-24 09:47:00

Mababa wa Sinodi wanalenga kushikamana na familia katika maisha na utume wake!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican akizungumza na waandishi wa habari, Ijumaa tarehe 23 Oktoba 2015 ameonesha kuridhishwa kwa Mababa wa Sinodi na kazi iliyofanywa na tume maalum ya kuhariri hati ya mwisho ya Mababa wa Sinodi itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko. Muswada umefanyiwa kazi na kuboreshwa zaidi, ikilinganishwa na hati ya kutendea kazi yaani “Instrumentum Laboris.

Maadhimisho ya Sinodi yamejikita katika ukweli na uwazi na kila mjumbe alikuwa huru kueleza yale yaliyokuwa moyoni mwake, akasikilizwa kwa makini na kuheshimiwa pasi na magomvi wala kinzani. Lengo lilikuwa ni kuziwezesha familia kushikamana katika upendo kwa kuzingatia mpango wa Mungu katika maisha yao. Mababa wengi wanaonesha matumaini kwa maadhimisho ya Sinodi ya familia ambayo imekuwa ni safari ya miaka miwili, ili kuliwezesha Kanisa kuchambua kwa kina na mapana wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu hati ya mwisho kutoka kwa Mababa wa Sinodi anakaza kusema, huu ni muhtasari wa mawazo makuu yaliyooneshwa na Mababa wa Sinodi na wala hakuna makundi yanayopingana wala kusigana; bali Mababa wa Sinodi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wana mawazo, mielekeo na vipaumbele vinavyotofautiana katika maisha na utume wa familia.Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika uelewa wa watu wenye mielekeo ya ushoga Ulaya na Marekani! Mwanzoni, hali hii ilionekana kuwa ni ugonjwa uliokuwa unatakiwa kupatiwa tiba, lakini kwa sasa mambo yamebadilika, ushoga linaonekana eti kuwa ni jambo la kawaida na sehemu ya maisha ya baadhi ya wananchi wa Ulaya na Marekani.

Lakini ikumbukwe kwamba, ushoga na ndoa za watu wa jinsia moja si sehemu ya mpango wa Mungu kwa ajili ya familia, ingawa watu wenye mielekeo kama hii wanapaswa kuheshimiwa pia. Bara la Afrika ambalo hadi sasa sehemu kubwa ya watu wake hawashabikii ushoga si kwamba wamepitwa na wakati au kundi linalopaswa kutupiwa madongo ya lawama!

Mababa wa Sinodi wanahitimisha majadiliano yao na waandishi wa habari kwa kukazia kwa mara nyingine tena umuhimu wa familia kama kiini na kitovu cha Uinjilishaji mpya. Kanisa ni nyumba ya wote inayokusanya wema na mabaya ambao wako tayari kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata upendo, msamaha na neema. Familia za Kikristo zinahamasishwa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Kanisa linatambua dhamana yake ya kuonesha ukarimu na wala si kuhukumu; Kanisa linalohudumia kwa haki, upendo na huruma, hasa kwa familia zenye migogoro na kinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.