2015-10-24 09:07:00

Maadhimisho ya Sinodi yanaridhisha!


Mababa wa Sinodi ya familia wamekamilisha muswada wa hati itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuitendea kazi kama sehemu ya mchango wa Mababa wa Sinodi katika wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, ameamua kuanzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Baraza hili jipya linachukua nafasi ya Baraza la Kipapa la Walei, Baraza la Kipapa la familia pamoja na Taasisi ya kipapa kwa ajili ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema ameunda tume maalum ambayo ameipatia dhamana ya kuandaa nyaraka muhimu zitakazojadiliwa na Baraza la Makardinali katika kikao chao, kitakachofanyika mwezi Desemba.

Wakati huo huo, Mababa wa Sinodi wamechagua wajumbe kumi na wawili wanaounda Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu. Mababa wa Sinodi wametambulishwa pia tume iliyoundwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kuhariri muswada wa Hati ya Mababa wa Sinodi kwa kuzingatia dhana ya Kanisa kutembea kwa pamoja, yaani kujikita katika maadhimisho ya Sinodi pamoja na kuzingatia ushauri na tafakari zilizotolewa na Mababa wa Sinodi. Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kuupitia muswada huo, tayari kuupigia kura na hatimaye, kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Mababa wa Sinodi wamegusia pia shida na mahangaiko ya familia nyingi huko Mashariki ya Kati na kwamba, Mababa wa Sinodi wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na kuendelea kuwatia moyo, ili waendelee kusonga mbele katika mshikamano wa upendo na uaminifu katika maisha ya kifamilia, licha ya changamoto zote hizo wanazokabiliana nazo!

Kimsingi maadhimisho ya Sinodi ya familia yamejikita katika umoja unaofumbata utofauti; ukweli, uwazi, upendo na mshikamano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kuendeleza dhana ya familia kama ilivyochambuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linataka kuwa ni mwenza wa familia katika hija yake ya maisha ya kiroho na kimwili, ili kuisaidia kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Kanisa linataka kushirikisha utume wake kwa familia, kwa kutoa ujumbe makini unaojikita katika ujasiri, wema, ukarimu na matumaini hususan kwa familia zinazoogelea katika mtikisiko wa imani. Lengo ni kutangaza Injili ya familia pamoja na kuziwezesha familia kuwa kweli ni mwanga wa mataifa. Kanisa linataka kupyaisha mikakati na sera zake za shughuli za kichungaji, kwa kujikita katika majadiliano na familia zenye kinzani.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kukazia umuhimu wa Kanisa kujenga na kuimarisha ari na moyo wa Sinodi, kwa kutembea pamoja, huku wakiheshimiana na kusikilizana hata katika tofauti zao, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa Kanisa la Kristo. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kujenga na kuendelea kuimarisha utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kutoa nafasi kwa Familia ya Mungu kushirikisha mawazo, matumaini na mashaka yake; tayari kufanyiwa kazi na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Maadhimisho ya Sinodi katika kipindi cha miaka miwili, imekuwa ni fursa muhimu sana kwa Kanisa katika kupembua wito na utume wa familia katika Kanisa na ulimwengu mamboleo.

Waamini walei wamechangia sana katika tafakari zao kama mashuhuda wa Injili ya familia na kwamba, hii ni changamoto kwa familia za Kikristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia kama walivyokuwa akina Aquila na Priscilla au familia ya Mtakatifu Martin na mtoto wao Mtakatifu Theresa wa Lisieux, waliotangazwa kuwa watakatifu na Papa Francisko, Jumapili ya tarehe 18 Oktoba 2015.

Maadhimisho ya Sinodi yaliyojikita katika ukweli na uwazi; umoja na utofauti, yamegusia mada mbali mbali kama vile: ndoa na talaka; Ekaristi Takatifu na wanandoa waliotalakiana wakaamua kuoa au kuolewa tena; tasaufi ya maisha ya familia; dhamiri nyofu, sheria na kanuni maadili; majiundo makini ya mihimili ya Uinjilishaji ndani ya Kanisa; familia zenye wagonjwa na walemavu; wakimbizi, wahamiaji; dhuluma na nyanyaso kwa familia za Kikristo pamoja na watu wenye misimamo na mielekeo ya ndoa za watu wa jinsia moja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.