2015-10-24 12:01:00

Kanisa la Mt. Gaspar, Mbezi Beach latabarukiwa na Kardinali Pengo!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi tarehe 24 Oktoba 2015 ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Gaspar del Bufalo, muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu. Tukio hili limefanyika wakati Shirika hili linaadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar alipoanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, ambalo leo hii lineenea sehemu mbali mbali za dunia, ili kusikiliza na kujibu kilio cha damu! Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanaadhimisha takribani miaka 50 ya uwepo na ushuhuda wao wa kitume nchini Tanzania na kwa namna ya pekee kwa kuzindua Kanda ya Tanzania, tukio ambalo lilifanyika hapo tarehe 8 Agosti 2015, Jimbo kuu la Dodoma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Ibada ya kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Gaspar na Kituo cha hija, Jimbo kuu la Dar es Salaam zilianza hapo tarehe 23 Oktoba 2015 kwa Ibada ya Rozari Takatifu na kufuatiwa na Masifu ya Jioni, ili kuomba rehema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aiwezeshe Familia ya Mungu Parokia ya Mt. Gaspar, kuwa kweli ni mahekalu hai na mashuhuda wa Injili ya familia, Kanisa dogo la nyumbani; shule ya utakatifu, haki na amani pamoja na kutambua kwamba, familia ni chemchemi ya miito mitakatifu. Kardinali Pengo ametabaruku Kanisa hili, tarehe 24 Oktoba 2015. Itakumbukwa kwamba, ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Gaspar ambalo kwas asa ni kituo cha hija Jimbo kuu la Dar es Salaam ulikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mtakatifu Gaspar del Bufalo alipotangazwa kuwa Mtakatifu kunako tarehe 12 Juni 1954 na Papa Pio XII.

Ifuatayo ni risala ya Parokia ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo na Kituo cha hija, Jimbo kuu la Dar es Salaam mbele ya Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, wakati wa kutabaruku Kanisa hili ambalo kwa kiasi kikubwa limechagiwa na Wamissionari wa Damku Azizi ya Yesu! Parokia ya Mt. Gaspar ilikuwa ni Kigango cha Parokia ya Mt. Nicholous Kunduchi Beach Mtongani kwa muda mrefu chini ya uongozi wa Maparoko wafuatao: Padre Dominico Altier C.PP.S, Padre Denis Massawe, C.PP.S na Alphonsi Minja, C.PP.S. Kutokana na uongozi wa Jimbo; Baba Kardinali Askofu Mkuu wa Jimbo aliamua Kigango hiki  kuwa Parokia. Utekelezaji wake ulianza  mnamo tarehe 11. 03. 2007 siku ya Jumapili ya tatu ya Kwaresma. Mnamo saa 2.00 asubuhi vifijo na nderemo na vigelegele vilisikika eneo lote la Kanisa Katoliki la Mt Gaspar del Bufalo na kituo cha hija.

Tukio kubwa la siku hiyo ilikuwa ni kutangazwa kwa Kigango cha Mt. Gaspar Del Bufalo Mbezi Beach, katika jimbo kuu la Dar Es Salaam kuwa Parokia.  Parokia hii ya Mt. Gaspar Del Bufalo ilipotangazwa na Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo, Mkuuu wa Shirika Kanda ya Italia Padre Giovanni Francilia, na Mkuu wa Shirika la Damu Azizi Vikarieti ya Tanzania Pd. Joachim Ndelianarua (ambaye kwa sasa ni marehemu) pamoja na Mapadre wengine washirika na Parokia za jirani walishiriki katika mashangilio hayo. Pia Paroko mwasisi wa parokia nyingi za Dekania ya Mt. Gaspar Padre Dominico Altier C.PP.S na  mwanzilishi wa ujenzi wa Makanisa kadhaa katika sehemu mbalimbali kama: Tegeta, Mtongani, Mt. Dominico Mbezi Juu, Bikira Maria wa Mama wa Huruma, Mt. Augustino Salasala alihudhuria uzinduzi wa Parokia ya Mt Gaspar Del Buffao.

Aidha katika siku hiyo, Baba Mwadhama, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam alimtangaza rasmi Padre Gregory Mkhotya kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia hii. Hivyo Paroko alianza rasmi majukumu yake ya kuisimamia Parokia hii kama inavyostahili kwa kuendeleza yale yote ya kiroho na kimwili katika Parokia hii na Kituo cha Hija kwa heshima ya Mt. Gaspar del Bufalo kwa kuishi kauli mbiu ya Mt. Gaspar kuwa “Kwa Mungu tufanye mengi, vizuri na haraka”. Hivyo alianza na kamati mpya ya Parokia kwa kufanya vikao mbalimbali na tarehe 13 /3/2007 kikao cha kwanza cha Kamati Tendaji kilikaa pamoja na Baba Paroko mpya kuweza kufahamiana pamoja na kupanaga mikakati mbalimbali ya kuendesha Parokia.

Waliohudhuria kikao hicho ni:       

  1. Mwenyekiti:                           Nd. Laurent Kalungira
  2. Mwenyekiti Msaidizi               Nd. Thaddei Mlingi    
  3. Katibu                                     Nd. Florian Ngunangwa (Udhuru)
  4. Katibu Msaidizi                       Nd. Agness Shengena  (Hawa Walikuwa Wamefiwa)
  5. Mhazini                                   Nd. Petronilla Lawi (Alifika)

 

MAKAZI YA MAPADRE:

Ili kurahisisha huduma za kiroho na utendaji mahiri na fasaha wa kazi za kitume katika parokia hii mpya na kituo cha hija waamini wakishiriiana kwa pamoja mapadre walitekeleza jukumu la kuwa na nyumba ya mapadre karibu zaidi na Parokia jamba ambalo lilifanyika kwa haraka kabisa. Hivyo mnano tarehe 7 March, 2008 uzinduzi rasmi wa nyumba ya Mapadre ulifanyika. Nyumba ambayo ilishaanza kutumika tangu tarehe 12/07/2007. Uzinduzi huo uliongozwa (na wewe) Baba Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo pamoja na Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu hapa Tanzania wanakamilisha adhima ya uzinduzi rasmi na kubariki nyumba ya Mapadre shughuli ambayo ilitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali nje na ndani ya Parokia.

Mwaka 2008 Parokia ya Mt. Gaspar ilipata Paroko Msaidizi ambaye ni Padre Patrick Athanas Kimaro C.PP.S ambaye alishirikiana bega kwa bega  na Paroko kuhakikisha kuwa shughuli zote za Parokia zinafanywa kwa ufanisi kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.  Mnamo mwaka 2010 Paroko aliyekuwepo yaani Padre Gregory Mkhotya C.PP.S alichaguliwa kuwa Msaidizi wa Mkuu wa Shrika hapa Tanzania. Mwaka 2010 kutokana na kuchaguliwa huko Padre Patrick Athanas Kimaro aliteuliwa rasmi na halmashauri ya Shirika kuwa Paroko wa Parokia hii na kituo cha hija akiendelea kuishi kauli mbiu ya Mt. Gaspar del bufalo yaani:

 “Kwa Mungu ni lazima tufanye mengi, upesi na vizuri. Mengi kwa sababu anastahi hivyo. Upesi kwa sababu maisha ni mafupi na vizuri kwa kuwa hiyo ndio njia ya pekee ya kumtumikia Mungu”. Haya ni maneno ya Mt. Gaspar del Bufalo. Baba Kardinali, kwa kuendeleza kazi za kitume chini ya ungozi wa Paroko Pd. Patrick akishirikiana bega kwa bega na Kamati Tendaji na Halmashauri ya Parokia na waamini wote. Kamati tendaji hiyo ni:

  1. Mwenyekiti                                     Nd. Adatus Kapesa,
  2. M/Kiti Msaidizi                      Nd. Augustino Shio,
  3. Katibu                                    Nd. Michael J. Kironde,
  4. Katibu Msaidizi                      Nd. Agness Shengena (Mrs),
  5. Mweka hazina                        Nd. Julius Rutabanja,
  6. Mhazini Msaidizi                    Nd. Petronila Lawi (Mrs).

KIGANGO:

Mnamo 04/04/2010 Kigango cha Mt. Thomas More kilikabidhiwa kwa Parokia ya Mt. Gaspar Del Bufalo kutoka Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma na Mwadhama Kardinali Pengo. Mwaka huu kigango kilipiga hatu na kutangazwa kuwa Parokia na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hapo tarehe 6.01.2015. Kwa sasa Parokia hii haina Kigango.

PAROKIA YA MT. GASPARI DEL BUFALO KWA SASA:

  1. WAHUDUMU/MAPADRE WA KIROHO

Baba Mwadhama, wahudumu wanaofanya kazi na Utume wa Parokia hii ni Mapadre Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristu. Idadi yao ni Wamisionari watatu (3) ambao ni:

  1. Paroko                    Pd. Patrick Athanas Kimaro,
  2. Paroko Msaidizi       Pd. Denisi Masawe
  3. Pd. Thomas Temba Kilewona.

 

  1. MISA TAKATIFU NA SALA HAPA PAROKIANI

Kwa kawaida hapa Parokiani kuna Misa nne (4) kila Jumapili. Na hii ndio ratiba ya huduma hapa parokiani kwetu:

 

JUMATATU – IJUMAA

MISA: SAA 12:15 ASUBUHI

 

JUMAMOSI NA SIKUKUU

MISA. SAA 1:00 ASUBUHI

 

JUMAPILI MISA

YA KWANZA SAA 12:00 ASUBUHI

YA   PILI SAA 1:00 ASUBUHI

YA TATU SAA 3:00 ASUBUH

YA WATOTO SAA 5:00 ASUBUHI

 

  1. KUABUDU

KILA ALHAMIS

12:45 ASUBUHIU – 12:30 JIONI

 

  1. MAUNGAMO

KILA JUMAMOSI

SAA 2:00 – 3:00 ASUBUHI

SAA 10:00 JIONI – 12:00 JIONI

 

  1. HUDUMA ZA OFISI

JUMANNE – JUMAMOSI

SAA 2:30 – 6:00 MCHANA

SAA 10:00 – 12:30 JIONI

JUMATATU OFISI HAZIFUNGULIWI ISIPOKUWA KWA SHIDA YA DHARURA

NB: Matayarisho ya ndoa yanafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu, ili kutoa nafasi kwa wanandoa kutambua wito na utume wao ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, kama ambavyo Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia wanakaza kusema. Lengo ni kuwasaidia wanandoa katika maisha yao kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia.

HUDUMA ZA KIROHO NA SAKRAMENTI

TAREHE 19/08/2008

Kwa mara ya kwanza Kanisa Katoliki la Mtakatifu Gaspari ikiwa kama Parokia kulitolewa Sakaramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 49, na Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo akishirikiana katika maadhimisho hayo na Paroko wa Parokia hii Baba Paroko Gregory Mkhotya,  Katika mahubiri yake Baba Mwadhama aliwaasa waimarishwa kuwa waalimu katika familia zao na jamii kwa ujumla katika kumtangaza Kristo aliye chimbuko la Upendo.

Baada ya misa waimarishwa walipokea vyeti pamoja na zawadi ya kitabu kiitwacho “Jifunze Kusali” Kitabu hiki humsaidia mwimarishwa kusali kwa ajili yake na wengine. Baada ya Misa Takatifu Baba Mwadhama alipata chakula cha mchana pamoja na waimarishwa.  Aidha, Parokia ilimzawadia Baba Mwadhama zawadi mbalimbali kwa ajili ya Seminari na shuguli nyingine za kichungaji. zawadi hizo ni Matoleo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maharagwe, mchele, unga, mafuta ya kupikia pamoja  na sadaka.

Baada ya kutolewa Sakramenti hii mwaka 2008 parokia ilizidi kukua na kuanza kutoa Sakaramenti zifuazo kwa mara ya kwanza:

        Ubatizo idadi; tokea mwaka 2008 hadi sasa ni watoto kwa watu wazima 279

  1. Ekaristi ni watoto 486.
  2. Kipaimara tokea mwaka 2008 hadi sasa ni watoto kwa watu wazima ni 735 waliopata sakaramenti hii.
  3. Ndoa tokea mwaka 2008 mpaka sasa ndoa zilizofungwa ni 150.
  4. Daraja takatifu:

Katika Parokia yetu tumepata upendeleo mara mbili kuandaa Upadrisho kama ifuatavyo:

  1. Mwaka 2008 tulipata bahati kuandaa Sakramenti ya Daraja takatifu kwa Wamisionari wa Damu Azizi sita (6).
  2. Mwaka 2013 tulipewa pia upendeleo kuandaa upadrisho kwa Mapadre wa hapa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wapatao sita.Tunamshukuru Mungu kwa neema hii.
  3. Huduma kwa wagonjwa hutolewa kila Ijumaa na Sakramenti zinazo husu wagonjwa hutolewa kama kawaida.

 

WAFANYAKAZI

Parokia ina wafanyakazi wafuatao: Masista 3, Makatekista 2,  Usafi wa mazingira 4, Wapishi 3, Mlinzi 1 na Walinzi ambao pia ni Kampuni ya Bahari Beach Security.

WAAMINI WA PAROKIA

(a) Waamini/wakristo: Paroki hii ina jumla ya waamini 2580.

(b) Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni 30.

(c) Vywama vya Kitume: ina vyama vya kitume tisa (9); WAWATA, UWAKA, VIWAWA, Utumishi wa Altare (Ministarant), Utoto Mtakatifu, Utume wa Fatima, Ushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mt. Anna na Legio Maria. (d) Vikundi vya Kiroho kiliturujia/ibada:             ina jumla ya Vikundi vya Kiroho vinne (4) ambavyo ni Utume wa Damu Azizi, Charismatiki Katoliki, Wasomaji wa Masomo kanisani, Kwaya ya Mt. Gaspar na Mt. Maria de Mattias.

HALI YA PAROKIA KWA SASA

Baba Mwadhama tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu hadi kufikia siku ya leo kwa mengi aliyotukirimia katika Parokia hii na kituo cha Hija, na hasa kwa siku ya leo iliyojaa furaha isiyo na kifani kwa Kanisa hili na Altre yake Kutabarukiwa. Kwetu sisi na wanajimbo wote tarehe ya leo 24.10.2015 imekuwa ya kihistoria kwa Kanisa la Mungu Duniani kote kwa Baraka tulizopata. Tunaahidi kujitahi kuendelea kulisha roho zetu na chakula cha kiroho na kutumia kwa makini Nyumba hii ya Mungu kwa Sala na Ibada. Aidha tunaahidi kutunza mahali hapa Patakatifu kwa hali na mali kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anazidi kuneemeka kiroho zaidi katika mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu.

Baba Mwadhama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Waaamini wa Mt. Gaspar del Bufalo wamekuandalia zawadi, tunakuomba uzipokee.  Mungu akubari siku zote za Maisha yako na kwa maombezi ya Mt. Yoseph Msimamizi wa Jimbo letu na Mt. Gaspar Del Bufalo somo wa Parokia yetu tunakutakia Utumishi wenye furaha na mafanikio.

Bikira Maria wa Damu Azizi akuombee.

Mt. Gaspari akuombee.

ITUKUZWE DAMU AZIZI YA YESU.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.