2015-10-24 12:29:00

Askofu mkuu Gualtieri, Balozi wa Vatican Mauritius; Pd. Gonsalo Askofu mpya!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Paolo Rocco Gualtieri kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini Mauritius. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Gualtieri, alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Madagascar na kwenye Visiwa vya Ushelisheli.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Aristide Gonsallo kutoka Jimbo kuu la Parakou, Benin kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Porto Novo, nchini Benin. Askofu mteule alizaliwa kunako tarehe 4 Septemba 1966. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapadrishwa kunako tarehe 27 Desemba 1992. Kati ya mwaka 1992 hadi mwaka 1997 alikuwa ni mwalimu Seminari ndogo ya Jimbo kuu la Parakou.

Kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2001 alipelekwa na Jimbo masomo ya juu katika Chuo kikuu cha Angers na kurejea nchini Benin kunako mwaka 2001 na kuendelea kufundisha Seminari ndogo ya Parakou. Kunako mwaka 2003 hadi mwaka 2004 alijiendeleza kwenye Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Angers kilichoko nchini Ufaransa na kujipatia Shahada ya uzamivu kwenye taalimungu na kurejea tena kuendelea kufundisha Seminari ndogo.

Kunako mwaka 2008 hadi mwaka 2012 alipelekwa tena Chuo kikuu cha Angers na huko akajipatia shahada ya uzamili na uzamivu. Kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2015 akateuliwa kuwa Paroko na mhudumu wa wagonjwa Hospitali ya Jimbo pamoja na kuwa ni mratibu wa huduma za afya Jimbo kuu la Parakou. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Porto Novo limekuwa wazi kutokana na kifo cha Askofu Renè-Marie Ehuzu, kilichotokea kunako tarehe 12 Oktoba 2012.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.