2015-10-23 09:35:00

Acheni ushabiki wa kisiasa na mafungamano mepesi mepesi ili kupata viongozi bora


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anawaalika watanzania kuonesha ukomavu unaovuka mipaka ya ushabiki na mafungamano mepesi mepesi ya vyama, kabila na dini, kwa kuongozwa na vipaumbele halisi. Watanzania kamwe wasisikumwe na ushabiki wa vyama na watu na badala yake watazame: malengo, mahitaji, changamoto na vipaumbele vya kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote!

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, lengo ni kulipatia taifa viongozi makini, wazalendo, wenye upeo mpana; watu wanaothubutu, tayari kushughulikia mafao ya wengi; kutetea, kulinda na kudumisha haki, amani na ustawi wa wote bila ubaguzi. Kwa namna ya pekee, anawataka watanzania kuhakikisha kwamba, wanafanya uchaguzi kwa amani na utulivu. Vyombo vya dola viwasaidie watanzania kutekeleza zoezi hili la kiraia kwa heshima na uhuru kamili bila kuegemea upande wowote. Vyombo hivi viwajengee wananchi mazingira mazuri ya kutekeleza uhuru wao kikatiba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.