2015-10-22 08:28:00

Wapambe nuksi! Bartimayo kipofu machachari aliyewatoa jasho wapambe wa Yesu!


Jumapili iliyopita tulitafakari habari juu ya tamaa ya mamlaka na madaraka. Na Yesu akaingiza dhana ya utumishi kwa yule anayetamani mamlaka na madaraka.Katika somo la kwanza tunasikia habari juu ya kikundi kidogo cha watu waliotoroka toka utumwa wa Waasiria. Utumwa umewabana na wametakaswa na kuwa wapya. Kwa njia ya mateso, watu wamekuwa wanyenyekevu na wamemgeukia Mungu kwa moyo wa toba. Walikuwa na vifungo vya mwili, kwa njia ya mateso, sasa wamepata mwono wa kiroho na kwa ufunguo huu wanaweza kumwona Mungu. Katika furaha yao hiyo, waliimba, kupiga kelele na kumshukuru Mungu aliyewafungua vilema, maskini, wenye watoto na wanaojifungua toka vifungo vya mwili. Mungu akawapa uhuru wa kiroho.

Katika somo la pili tunaona kuwa kila kuhani mkuu anatoka kwa watu ili kumtumikia Mungu na watu wake. Wao na watu wanaendelea kujitakatifuza. Kazi ya kuhani mkuu ni wito wa Mungu, kama haruni. Mtume Paulo anaelezea vizuri utume huu katika 1Kor. 4 ... anapoongea kuhusu huduma ya mitume kama watumishi.

Katika Injili, tunaambiwa kuwa Yesu ameteuliwa na Mungu ili kuokoa watu na kuwapatia msamaha wa dhambi. Leo tunasoma sehemu ya Injili juu ya habari ya uponyaji wa Bartimayo. Habari hii ya uponyaji wa Bartimayo inawagusa wasomi wote wa maandiko matakatifu kwa vile ni mahali pekee katika Injili pacha, jina la mtu aliyeponywa linaandikwa. Tena linatajwa mara mbili. Si kawaida kutaja jina la aliyeponywa katika Injili.

Katika lugha za Kiaramayo, jina lilikuwa ni zaidi ya bango. Jina lilieleza utu wa mtu na hali yake yote. Jina la mtu ni mtu mwenyewe. Ndivyo ilivyo pia katika mila na desturi za kiafrika. Jina ni mtu mwenyewe na unaweza kumfahamu mtu au mila na desturi zake au mahali anapotoka au kipindi alichozaliwa ukijua jina lake. Yawezekana ikawa katika lugha ya Kiaramayo alipewa jina hili kwa kuwa alikuwa kipofu na katika mazingira yao upofu ni adhabu toka kwa Mungu – Yoh. 9:34. Uelewa wa Kigiriki wa jina hili ulimaanisha aliye na baraka. Na hii yaonesha utu wake halisi. Ni kwa nini Marko atupe jina la mtu lenye maana mbili tofauti? Laana na Baraka? Wataalamu wanasema Yesu anaingia hapa ili arudishe si tu hali yake ya nje bali pia adhihirishe ndani yake na wengine ukuu wa Mungu aliye mwuumba wake. Yesu alimwezesha kujitambua.

Ni vizuri leo tukaangalia tena hali zetu kimwili na kiroho. Tukoje? Tunajitambua? Tunaomba nini kwa Yesu? Ili tuombe ni lazima kujitambua na kuelewa kile tunachokiomba. Tunaomba kuona? Kwani sisi ni vipofu? Wa nini? Halafu iwe nini? Wakati mwingine inabidi tufikirie vizuri sana. Je, Bartimayo alikuwa kipofu (blind) au alikuwa na shida ya uoni hafifu (sightless)? Yeye katika hali yake na kwa jinsi alivyokuwa kwamba ni kipofu au alikuwa na uoni hafifu aliweza kutambua kilichokuwa kinaendelea katika mazingira yake. Kwamba Yesu anapita na akaomba apate kuona. Tena kwa kelele kiasi kwamba inakuwa kero kwa wengine. Sasa vipofu ni wepi? Wenye macho ambao hawatoi ombi lo lote kwa Yesu ingawa yupo au anapita kati yao au yule ambaye haoni kwa macho lakini anatambua uwepo wa Kristo? Ingawa haoni kwa macho yake, anaweza kuona toka rohoni mwake. Tutafakari sana.

Mimi binafsi nina mfano hai na wa kweli, wa kipofu aliyenitambua baada ya kuachana miaka 10 iliyopita. Alifika kumwona ndugu yake katika jumuiya yetu. Kumbe pia nilimpatia lifti kwenye gari yangu na kumsindikiza stendi. Nilikutatana naye miaka kumi (10) baadaye. Hakika yeye ndiye aliyenitambua, tena vizuri kabisa na kuelezea mazingira tuliyokutana na msaada niliompatia. Mimi nilifanya kazi ya kumkumbuka, yeye alinikumbusha matukio ili inisaidie kukumbuka mazingira tuliyokutana. Ajabu kweli. Nilijisikia vibaya kweli. Ilikuwa changamoto kubwa kwangu mimi mwenye macho mazima.

Tutafakarishwe tena na mfano huu. Ilitokea katika monasteri moja watawa wake walipoteza dira na kuishi bila kuwa na roho wa Mungu ndani yao. Kila mmoja akaishi kivyake. Maisha yakawa magumu kweli kweli kati ya watawa wale. Miito ikakatika kabisa na hata wengi kati ya waliokuwa ndani wakaondoka. Kila siku jioni mbele ya monasteri yao alikuwa akipita mzee mmoja akienda sehemu fulani porini kusali. Watawa wachache waliobaki wakamshauri abate wao aongee na huyo mzee kuhusu hali yao mbaya.

Baada ya kufanya hivyo na kukutana na yule mzee na kumsimulia hali yao akampatia ushauri. Akamwambia kati yenu yupo Yesu. Abate akashangaa sana kwa neno hilo. Abate aliporudi Monasterini watawa walikuwa na hamu ya kujua kapewa ujumbe gani. Akawaeleza mazungumzo aliyofanya na yule mzee na kuwa amemwambia kuwa kati yao Yesu yupo. Changamoto hii ilikuwa kubwa sana kwa watawa wale. Tangu siku hiyo wakaanza kuangaliana kwa namna ya pekee na kuanzia hapo maisha yao yakabadilika kabisa. Wakakumbuka kuwa wanatakiwa kumtumikia Yesu na si wao wenyewe. Kumbe waliishi bila Yesu, wakamweka pembeni. Wakapoteza mwelekeo.

Je, Yesu yukoje leo na wakati wetu huu katika roho zetu, katika maisha yetu, katika familia zetu, katika jumuiya zetu katika kigango chetu, katika parokia yetu na katika taifa letu? Je ni mazingira gani yaweza kutuashiria ili tutambue kama Bartimayo kuwa Yesu yupo au anapita katika maeneo yetu ili tumwite atusaidie kuona tena?

Hakika hatuna budi kuwa na macho zaidi ya kiroho. Kama Bartimayo ni lazima tumwite Bwana, nifanye nione na tukipata kuona, tumtangaze huyo Kristo mwokozi wetu. Mtume Paulo katika  1Kor. 3:19 – anasema, kwa maana hekima ya ulimwengu hu ni ujinga mbele ya Mungu, kwani imeandikwa: yeye huwanasa wenye heima katika hila yao. Hatuna budi kuvuka hekima yetu na katika kuishi kwetu tuiite hekima ya Mungu ili itusaidie kumtambua Mungu aliye ndani yetu na kati yetu.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.