2015-10-22 07:38:00

Maadhimisho ya Sinodi ni tukio endelevu katika maisha na utume wa Kanisa!


Mababa wa Sinodi wanasema, maadhimisho ya Sinodi ni changamoto endelevu inayogusa maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya ndoa na familia; ni changamoto inayofumbatwa katika Mafundisho tanzu, Sakramenti na Nidhamu ya Kanisa. Utume wa Kanisa kwa ajili ya familia unapaswa kutekelezwa kwa kufumbatwa katika fadhila ya upendo, uvumilivu; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Kushughulikia familia zinazoteseka kutokana na myumbo wa imani na maadili kwa ujasiri, hekima, busara, ukweli, huruma na mapendo.

Mababa wa Sinodi katika muhtasari wa tafakari za makundi madogo madogo mintarafu sehemu ya tatu ya hati ya kutendea kazi, Instrumetuma Laboris kuhusu utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo wanakaza kusema, Injili ya familia ni ujumbe unaopaswa kuwashirikisha Wakristo wote, ili waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika uhalisia wa maisha.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kusisitiza kwamba, utume wa familia utekelezwe kwa dhati kabisa kwa kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti; huruma na upendo ili kutoa nafasi kwa wanandoa wanaoishi katika matatizo ya kiimani kuonja tena huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao na hatimaye, kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Mapendekezo yatakayotolewa na Mababa wa Sinodi yaguse uhalisia wa maisha na kuangalia uwezekano wa kuyatekeleza katika uhuru unaowajibisha pamoja na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanatambua kwamba, matatizo, changamoto na fursa za maisha ya ndoa na familia hazina njia ya mkato, zinahitaji tafakari ya kina kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ndiyo maana Sinodi ni mchakato endelevu. Hii inatokana na ukweli kwamba, bado kuna mada tete ambazo zitaendelea kufanyiwa kazi, ili hatimaye, Kanisa liweze kupata muafaka. Tatizo la wanandoa waliotalakiana na hatimaye wakaamua kuoa au kuolewa wanaotaka kupokea Ekaristi Takatifu pamoja na watu wenye mielekeo ya ndoa za jinsia moja, ni kati ya mada ambazo hazina majibu ya mkato.

Wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena ni mada inayogusa Mafundisho tanzu ya Kanisa na kwamba, Sinodi za Maaskofu hazina uwezo wala madaraka ya kutengua mafundisho haya, dhamana inayoweza kutekelezwa na Mtaguso wa Maaskofu. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wanasema Kanisa linawajibu na dhamana ya kuwapokea, kuwasikiliza na kuwasindikiza wanandoa wenye shida na magumu ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika mchakato wa huruma ya Mungu au safari ya upatanisho kwa kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa. Wajibu huu unaweza kutekelezwa na Askofu mahalia na Mabaraza ya Maaskofu. Mababa wa Sinodi wanasema, Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Mites Iudex” unaweza kusaidia kuleta ufumbuzi kwa ndoa zenye migogoro katika kipindi cha muda mfupi, kwa kuzingatia Sheria na Mafundisho ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanatumaini huruma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kuwasaidia wanandoa kuanza mchakato wa safari ya upatanisho wa maisha ya kiroho, safari ya upendo au safari ya toba mintarafu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuunda Tume maaluma itakayolishughulia suala hili na kulipatia ufumbuzi kwa wakati muafaka. Watu wenye mielekeo ya ndoa za jinsia moja haikuwa sehemu muhimu sana ya maadhimisho ya Sinodi, kumbe, mada hii inaweza kushughulikiwa nje ya maadhimisho ya Sinodi kwa kuitisha mkutano maalum wanasema Mababa wa Sinodi ambao wanakaza kuhusu haki za watoto kuwa na baba na mama pamoja na kupata malezi makini.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kusema kuwa, familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya, kumbe ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa ndoa na familia kwa kukazia: majiundo, awali na endelevu yanayopaswa kutolewa hatua kwa hatua, kwa kujikita katika Neno la Mungu, Mafundisho tanzu ya kanisa na Sakramenti za Kanisa.

Kanisa liendelee kusoma alama za nyakati, kwa kuwa na lugha inayoelekwa na wengi inapofundisha, ili waamini waweze kutambua na kuthamini uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutolea ushuhuda Injili ya familia. Wanafamilia wazingatie Injili ya uhai, uzazi unaowajibisha katika makuzi na malezi ya watoto. Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, ndoa mchanganyiko ni mahali muafaka pa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuwasaidia waamini kutambua maisha ya familia yanayoweza kutikiswa na magonjwa pamoja na vifo. Kanisa liwasaidie waamini kuondokana na ndoa sugu kwa kujikita katika Sakramenti ya Ndoa.

Umaskini na hali ngumu ya maisha kwa wanandoa walioachana, vipigo na ukatili wa majumbani, mifumo dume; wakimbizi na wahamiaji; vita na kinzani ni mambo ambayo yanaendelea kutikisa msingi wa maisha ya ndoa na familia. Ni wajibu wa Kanisa kuwa kweli ni sauti ya wanyonge! Mababa wa Sinodi mwishoni, wanasema, sehemu ya tatu ya hati ya kutendea kazi inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa, kabla ya kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.