2015-10-21 10:29:00

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania kumekucha!


Waangalizi wa muda mfupi 60 kutoka Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) wameshawasili jijini Dar es Salaam ili kuangalia uchaguzi mkuu nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 25 Oktoba.  Watasambazwa nchini kote tarehe 20 Oktoba ambako wataungana na Waangalizi wa Muda Mrefu wa EU, ambao wamekuwa wakifuatilia maandalizi ya uchaguzi pamoja na kampeni tangu mwisho wa Septemba. “Kwa kuwapeleka Waangalizi wetu wa muda mfupi,

Ujumbe wa waangalizi wa EU utaongeza upeo wa uangalizi wake na utafuatilia shughuli siku ya uchaguzi,” alisema mwangalizi Mkuu wa EU, Judith Sargentini. “Tutakuwa na waangalizi 140 watakaotembelea vituo vya kupiga kura kwenye maeneo ya mijini na vijijini, kwenye mikoa yote, ili kuangalia upigaji na kuhesabiwa kwa kura. Waangalizi wetu watafuatilia pia uorodheshwaji wa matokeo, ambazo ni sehemu muhimu ya tathmini ya jumla ya EU EOM ya mchakato wa uchaguzi,” aliongezea Bi Sargentini. Kabla ya kupelekwa kwao, Waangalizi wa Muda Mfupi watapata maelezo ya kina Jijini kuhusu taratibu za uchaguzi, mfumo wa kisheria wa uchaguzi na hali ya kisiasa nchini Tanzania

EU EOM kwa Tanzania ndiyo ujumbe mkubwa wa waangalizi wa kimataifa nchini na utakaokuwepo nchini kwa muda mrefu zaidi, kati ya tarehe 11 Septemba na 15 Novemba. Ujumbe unahusisha kundi kuu la watathmini wa uchaguzi 10 waliopo Jijini na visiwani Zanzibar, waliowasili tarehe 11 Septemba; Waangalizi wa Muda Mrefu 34 waliowasili tarehe 24 Septemba ambao wako nchini kote; Waangalizi wa Muda Mfupi 60; ujumbe wa Wabunge 6 wa Bunge la Ulaya; na Waangalizi wa Muda Mfupi wa Ndani 30 watokanao na wafanyakazi wa kidiplomasia wa Ubalozi wa EU nchini Tanzaniapamoja na balozi za nchi wanachama wa EU, Norway, Uswisi na Canada.

EU EOM kwa Tanzania ilitumwa baada ya mialiko toka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. Jukumu la ujumbe huo ni kuangalia maswala yote ya mchakato wa uchaguzi na kutathmini ni kwa kiasi gani uchaguzi unafuata misimamo ya kimataifa na ya kikanda kuhusu chaguzi za kidemokrasia ilioridhiwa na Tanzania, pamoja na sheria za nchi. EU EOM itafanya kazi huru kutoka taasisi na nchi wanachama za EU. EU EOM itatoa tathmini yake ya awali ya uchaguzi kwenye mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya siku ya uchaguzi.

Na Thompson Mpanji,

Mbeya, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.