2015-10-21 09:12:00

Sinodi ni kielelezo cha umoja, upendo, ukweli na uwazi!


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia wanakabiliwa na changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa familia, ili kweli ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia; changamoto ambazo zinapaswa kupokelewa katika mwanga wa Injili, Mafundisho tanzu ya Kanisa, haki na huruma ya Mungu. Kardinali Jorge Liberato Urosa Savino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Caracas, Venezuela anasema, maadhimisho ya Sinodi yanafanyika katika hali ya umoja, upendo, mshikamano na udugu; katika ukweli na uwazi; katika umoja na utofauti; mambo ambayo yanaonesha kwa kiasi kikubwa Ukatoliki wa Kanisa.

Kardinali Savino anakaza kusema, leo hii familia zinakabiliwa na changamoto na matatizo makubwa kama vile: talaka, jambo linalotikisa msingi wa ndoa na familia; umaskini, hali ngumu ya maisha; ukosefu wa fursa za ajira; wahamiaji na wakimbizi; magonjwa na ugumba. Haya ni mambo ambayo yanaendelea kuangaliwa katika mwanga wa Injili ya familia inayokumbatia upendo na huruma ya Mungu katika ukweli na haki, ili kumwezesha Mwenyezi Mungu kuganga na kuponya madonda ya maisha ya familia kwa njia ya toba na wongofu wa ndani.

Ni dhamana na jukumu la Mama Kanisa kuzima kiu ya mwanadamu kwa kumpatia mwelekeo sahihi wa maisha kadiri ya mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa, bila kutelekeza: haki, ukweli na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mafundisho tanzu ya Kanisa ni amana na hazina ambayo Kanisa linapaswa kuishirikisha Familia ya Mungu. Ni matumaini ya waamini kwamba, Mababa wa Sinodi wataweza kutoa majibu muafaka kwa changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia, katika ukweli, uwazi na huruma ya Mungu.

Kardinali Savino anakiri kwamba, familia nchini Venezuela inakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kutoungwa mkono na wengi kutokana na dhamana na utume wake katika Jamii. Vijana wengi wanaogopa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kufunga Sakramenti ya Ndoa na kuishi kadiri ya amri na maagizo ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Makazi, ajira na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii ni kati ya mambo yanayoendelea kudhoofisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Mama Kanisa anaendelea kuwainjilisha watu ili kutambua na kuenzi uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kama kiini cha maisha ya kijamii, shule ya upendo na ukarimu; haki, amani na mshikamano wa dhati. Ni katika maisha ya kifamilia kwamba, watu wengi wanaonja ule upendo wa kidugu; imani, matumaini na ukarimu unaofumbatwa katika utashi mwema. Ni wajibu wa Kanisa na jamii kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na jamii kuendelea kuzijengea familia uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha. Badala ya kukata tamaa, familia zijenge utamaduni wa kumwilisha Injili ya matumaini katika safari ya maisha yao ya kila siku, huku zikijiaminisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Askofu Raphael Balla Guilavogui wa Jimbo Katoliki N’Zerèkorè, Guinea anakaza kusema, ndoa mseto kati ya Wakatoliki na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo ni changamoto na fursa kubwa ya kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene katika uhalisia wa maisha unaofumbatwa katika ukweli na uwazi. Wakati mwingine ndoa mseto zimekuwa ni chanzo cha mahangaiko makubwa katika familia kutokana na utofauti kati ya Sakramenti ya Ndoa na Ndoa katika dini nyingine.

Kwa mfano anasema, Waamini wa dini ya Kiislam wanaruhusiwa kuwa na wake zaidi ya mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha Sakramenti ya Ndoa. Katika jamii ambazo mfumo dume unatawala, watoto wanapaswa kusikiliza sauti ya baba wa familia, hili linaweza kuwa ni tatizo kubwa katika masuala ya Ibada. Changamoto zote hizi zinaonesha kwamba, Kanisa halina budi kukazia zaidi maandalizi ya wanandoa watarajiwa pamoja na kuendelea kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Injili ya Familia.

Kwa vile Kanisa ni Mama na Mwalimu, ni matumaini ya Mababa wa Sinodi kwamba, Kanisa litaweza kutoa neno la faraja kwa wanandoa za mseto, ili waweze kusonga mbele katika imani na matumaini licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo!

Wakati huo huo, Askofu mkuu Francisco Chimoio, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji anasema, wanandoa wanapaswa kufundwa ili kutambua, kuheshimu na kuenzi upendo, uzuri, utakatifu na udumifu wa maisha ya ndoa, tayari kupokea na kuwalea watoto kadiri ya mpango wa Mungu. Familia ziwe ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa kusikiliza Neno la Mungu na kulimwilisha katika matendo ya huruma; ni mahali pa ukarimu na msamaha, ari inayopata mwamko wake katika maisha ya Kisakramenti.

Familia nyingi nchini Msumbiji zimeguswa na kutikiswa na vita ya wenyewe kwa wenyewe na sasa zinaanza kuimarisha misingi ya umoja, upendo na mshikamano. Ni familia zinazokabiliwa na hali ngumu ya maisha pamoja na umaskini unaosababishwa wakati mwingine na majanga asilia; lakini bado zinaonesha ile furaha na utakatifu wa ndoa na ziko tayari kuwarithisha watoto wao imani na tunu msingi za maisha pamoja na mapokeo mazuri kutoka katika mila na tamaduni zao.

Utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia ni mambo mazuri, lakini wakati mwingine yana sababisha changamoto kubwa katika misingi ya maadili na utu wema; mambo yanayokumbatiwa na utamaduni wa kifo, ndoa za watu wa jinsia moja, mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Ukanimungu ni mambo yanayoanza kuingia pole pole katika mawazo na akili kwa baadhi ya wananchi wa Msumbiji. Lakini, Kanisa linawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Msumbiji kuenga msingi bora wa familia, shule ya utakatifu na utu wema kwa kuwa ni mashuhuda wa kweli wa Injili ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.