2015-10-21 09:35:00

Huruma ya Mungu, Mafundisho tanzu ya Kanisa; haki, ukweli na uwazi ni uhimu


Mababa wa Sinodi katika tafakari zao wakati wa maadhimisho ya Sinodi wameonesha umoja na kutofautiana katika baadhi ya mambo; lakini majadiliano yote haya yanafanyika katika misingi ya umoja, udugu na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu, inayohamasishwa kujikita katika ushuhuda wa Injili ya familia. Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sektretarieti ya Uchumi Vatican anasema Mafundisho juu ya huruma ya Mungu; Mafundisho tanzu ya Kanisa; ukweli, haki na uwazi ni mambo msingi ambayo Mababa wa Sinodi wanaendelea kuyakazia katika maisha ya ndoa na familia.

Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji unaojikita na kuambata huruma ya Mungu. Mafundisho tanzu ya Kanisa hayaguswi kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, bali ni kuendelea kufafanua utekelezaji wa huruma ya Mungu katika masuala ya nidhamu ya maisha ya Familia ya Mungu. Kanisa linataka kuwa na msimamo mmoja kuhusu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Sakramenti hii iwe ni kiungo cha umoja, chemchemi ya upendo na mshikamano na kamwe isiwe ni sababu ya kuwagawa waamini. Umoja wa Kanisa ujikite katika Mafundisho tanzu na Sakramenti za Kanisa, hasa kwa wanandoa waliotalikiana na kuamua kuoa au kuolewa tena. Mababa wa Sinodi, tangu mwanzo wameonesha umoja na tofauti zao; mambo ambayo yamefafanuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya Sinodi, ili kuwa na msimamo mmoja katika masuala nyeti, yanayoweza kuligawa na kulisambaratisha Kanisa.

Jambo la kutilia mkazo ni kuhusiana na : Mafundisho tanzu ya Kanisa, Sakramenti za Kanisa na Nidhamu. Sakramenti ya Ndoa ni muungano thabiti kati ya bwana na bibi katika kifungo cha upendo wa thati unaopania kupata watoto na kuwalea kadiri ya mpango wa Mungu. Ndoa za watu wa jinsia moja ni ukiukwaji wa mpango wa Mungu, watu hawa wanaweza kupokelewa na kusaidiwa bila kutengwa, kwani Kanisa ni Mama na mwalimu wa wote! Kanisa litaendelea kuwaelimisha watu wa mataifa kwa mwanga wa Injili na Mafundisho tanzu ya Kanisa yanayotekelezwa katika nidhamu na Sakramenti za Kanisa. Kanisa litaendelea kuwasaidia watoto wake wanaoogelea katika shida na mpasuko wa imani, ili kuwaganga na kuwaponya kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, ikiwa kama wataonjesha moyo wa toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.