2015-10-20 07:39:00

Yaliyojiri katika mahojiano na Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Paris Match anakiri kwamba, maandalizi ya hija za kitume pamoja na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kati ya mambo ambayo ameyapatia kipaumbele cha pekee katika miezi ya hivi karibuni na kwamba, kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Mwezi Septemba aliweza kutembelea nchini Marekani. Hakuwahi kufika huko kutokana na sababu za maisha na shughuli zake za kichungaji.

Familia ya Ludovico Martin na mke wake Maria Azelia Guèrin, waliotangazwa na Kanisa kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 18 Oktoba 2015, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku ya 89 ya Kimissionari Ulimwenguni ni kielelezo na mfano wa kuigwa na familia ya Mungu. Hawa ni wanandoa ambao wameshuhudia uzuri wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika maisha ya kifamilia. Ni familia ilionesha upendo na mshimamano wa dhati na maskini, kwa kuwaheshimu na kuwasaidia katika shida na mahangaiko yao. Ni familia ambayo ni kitovu na chachu ya ukarimu na Uinjilishaji, na matunda ya utume huu ni Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ana Ibada ya pekee kwa Mtakatifu Theresa wa Lisieux, mfano wa mwamini anayejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kujikita katika upendo wa Mungu unaofumbata upatanisho, unaopaswa kusambaa na kuenea kwa Kanisa zima. Ni mwamini makini katika maisha na maneno yake, anayeonesha mfano bora kwa mwamini kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ili aweze kuwa ni kiongozi na dira ya maisha. Katika shida na mahangaiko yake ya shughuli za kichungaji, Baba Mtakatifu anasema, huwa anapenda kumkimbilia Mtakatifu Theresa na kumkabidhi mahangaiko kwa imani na matumaini na kwamba, wakati mwingine amemsikiliza na kumkirimia maombi yake!

Baba Mtakatifu anasema, amemchagua Mtakatifu Francisko wa Assis kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake ya kichungaji kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kutokana na changamoto aliyopewa na Kardinali Claudio Hummes, baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa akamwomba, kamwe asiwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Francisko wa Assis ni kielelezo makini cha ufukara wa Kiinjili; mwamini aliyesimama kidete kulinda na kutetea amani; akawa ni rafiki mkubwa na mtunzaji wa mazingira, changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na waamini pamoja na wote wenye mapenzi mema.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuibua mbinu mkakati bora na inayowajibisha ili kulinda na kutunza mazingira, kwa ajili ya mafao ya wengi. Utunzaji bora wa mazingira ni chachu muhimu sana katika mchakato wa kupambana na baa la umaskini na njaa duniani. Sera na mikakati ya kimataifa itoe kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; ili kupambana na baa la njaa, umaskini, vita, ukosefu wa fursa za ajira na ubaguzi; tayari watu kuonesha mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mazingira ni nyumba ya wote inayopaswa kutunzwa, ili kuimarisha maisha ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na unafiki wa kisiasa kwa kuangalia hali halisi ya maisha ya binadamu, kwa kuwajali na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anapongeza juhudi na ugunduzi unaoendelea kufanywa na wanasayansi katika medani mbali mbali za maisha, haya yanapaswa kuwa ni matunda ya akili na upendo kwa Mwenyezi Mungu anayemtakia mema binadamu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wake na kumkomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo yanayopelekea kukimbia makazi na nchi zao ni jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho na Jumuiya ya Kimataifa. Uhuru wa kuabudu, rufuku ya biashara ya silaha; ukweli na uwazi kwa wanasiasa na wafanyabiashara, ili kweli amani na utulivu viweze kutawala duniani. Mikakati ya maendeleo ikitoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu badala ya fedha na faida kubwa, janga la wakimbizi na wahamiaji linaweza kupatia ufumbuzi wa kudumu. Familia ya Mungu ijikite katika upendo na huruma, kiini cha Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa jirani zao.

Vatican inaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika medani mbali mbali za kimataifa kwa kukazia diplomasia na majadiliano kama njia ya kutatuta suluhu ya kinzani na migogoro mbali mbali sanjari na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu. Mchakato wa haki, amani, upatanisho na ushirikiano ni mambo msingi katika kutafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahojiano maalum na Paris Match kwa kukazia kwamba, maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yawawakumbushe wahudumu wa Kanisa kwamba, wao ni vyombo vya neema, huruma na upendo wa Yesu kwa waja wake. Yesu Kristo mkombozi wa dunia ndiye anayepaswa kupewa heshima, sifa na utukufu. Anasema amana kubwa ambayo imeacha chapa ya kudumu katika moyo wake kutoka kwa Wayesuit ni ile kiu ya kutaka kumfahamu Kristo Yesu, katika uhalisia wa maisha sanjari na kumwilisha mafundisho yake, ili kujenga na kudumisha mahusiano mema na jirani. China bado iko bado moyoni mwake.

Anapenda bado kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa kukutana na watu mbali mbali huko barabarani, eneo ambalo Yesu alipenda kulitumia kwa ajili ya kutangaza Ufalme wa Mungu! Hi indi ndoto, kwani kwa hali ya kawaida kwa sasa jambo hili haliwezekani tena!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.