2015-10-20 08:24:00

Onesheni mshikamano wa hali na mali na Wakristo wanaoteswa na kudhulumiwa!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawapongeza wadau wote waliohusika kuandaa na hatimaye kuchapisha taarifa ya Mwaka ya Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, ACS kuhusu mateso, nyanyaso na madhulumu wanayofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Ni watu wanaoteswa na kusahauliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, hivi karibuni lilizindua taarifa yake ya mwaka kwa kuonesha kwa kina na mapana Wakristo wanavyonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia katika kipindi cha Mwaka 2013 hadi mwaka 2015. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wale wote wenye dhamana ya uongozi, kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo zinaondolewa katika uso wa dunia na badala yake, wanakuze uhuru wa kuabudu sanjari na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wataguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.