2015-10-20 14:01:00

Kumbatieni misingi ya haki, amani, usalama na majadiliano! Vita si mali kitu!


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana ban Ki-Moon katika ujumbe wake kwa njia ya video amewataka wananchi wa Israeli na Palestina kuondokana na chuki pamoja na hali ya kulipizana kisasi, mambo ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na badala yake wajikite katika misingi ya amani na usalama kwa wote, ingawa matumaini ya tunu hizi msingi yamekuwa yakivurugwa mara kwa mara kutokana na kinzani pamoja na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Ni jambo lisilokuwa na tija wala mashiko kwa vijana kukimbilia silaha na mawe wakiwa na nia ya kutaka kufanya mauaji ya kinyama! Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anatambua machungu na mahangaiko ya vijana wa Kipalestina katika mchakato wa kutafuta amani; anatambua hasira ya maeneo yao kukaliwa kwa mabavu na Israeli kuendelea kujenga makazi ya watu katika eneo la Palestina.

Katibu mkuu anawaambia viongozi wa Palestina kuanzisha mchakato wa amani miongoni mwa watu wao, ili ndoto na matamanio yao yaweze kufikiwa, kwani wanahaki ya kuheshimiwa, utu na uhuru wao kulindwa na kudumishwa. Hili ni lengo pia la Umoja wa Mataifa, kuhakikisha kwamba, Waisraeli na Wapalestina wanaishi kwa amani, upendo na mshikamano. Hii ni changamoto kwa viongozi wa kisiasa na serikali kuwajibika zaidi, kwa kutoa ulinzi na usalama kwa vijana wa kizazi kipya. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa kisiasa ili suluhu ya kweli iweze kupatikana.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anawataka vijana wa Palestina kuweka chini silaha za kukata tamaa; viongozi wa Israeli kujikita katika mchakato wa amani na usalama bila kutawaliwa na hasira, ili kuwapatia watoto fursa ya kwenda shule; watu kuwa na makazi salama, ili kuendelea kuishi kwa amani. Waisraeli na Wapalestina hawana budi kuvunjilia mbali mzunguko wa vita na woga, ili kujielekeza zaidi na zaidi katika majadiliano yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa.

Ni changamoto ya kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; mambo ambayo wakati mwingine yamekuwa ni kikolezo cha vurugu na mpasuko wa kijamii. Kila upande unawajibika kusimama kidete dhidi ya magaidi na vitendo vya kigaidi, kwa kushuhudia kwa maneno na matendo kwamba, maeneo ya kihistoria yaliyoko mjini Yerusalemu yatalindwa na kuheshimiwa. Viongozi wa pande zote mbili, wawe tayari kushughulikia ukosefu wa fursa za ajira hali inayopelekea vijana wengi kukata tamaa. Amani na utulivu ni dhamana inayojikita katika ujasiri, utu wema pamoja na kuwajengea vijana matumaini. Huu ndio ujasiri unaopaswa kuoneshwa na viongozi katika Nchi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.