2015-10-19 10:31:00

Watanzania salini na kufunga ili kuombea uchaguzi mkuu 25 Oktoba 2015


Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kumaliza salama utumishi wake Serikalini kwenye ngazi za juu ambao umedumu kwa takriban miaka 15.Akizungumza na waamini wa Kanisa Katoliki wakati wa Ibada ya Jumapili katika Parokia ya Mt. Anna iliyoko Hananasifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumapili, Oktoba 18, 2015, Waziri Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa; pia katika ngazi ya uwaziri miaka miwili na nusu na miaka mitano akiwa Naibu Waziri.

“Ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumaliza uongozi wangu Serikalini. Ninamaliza uongozi wangu kwa amani na furaha. Katika ibada hii ya shukrani nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi… yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi kujua,” alisema. “Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa Naibu Waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.

“Wito wangu kwa Watanzania wote ni kwamba msiache kumtanguliza Mungu maishani kwa sababu yeye ndiye mtoaji wa yote. Wote tuendelee kumtii Mungu na viongozi wetu wa kiroho kwa sababu wako hapa kumwakilisha yeye,” alisema. Alikaza kusema wako baadhi ya watu ambao wakipata madaraka wanaona kwenda Kanisani ni kero au ni kupoteza muda. “Tatizo lao ni kutojijua, hawatambui kwamba bila Mungu hizo nafasi wasingezipata. Ninawaomba tujue kwamba kuna maisha hata nje ya utumishi wa umma na utumishi wa kisiasa,” alisema.

Alisema katika utumishi wake wa umma amejifunza mambo mengi lakini kikubwa alichobaini ni kujua jinsi ya kuishi na watu. “Elimu kubwa ni kujua jinsi ya kuishi, hii ni elimu zaidi ya kitabuni,” alisema. Alitumia fursa hiyo kumshukru mke wake, Mama Tunu Pinda kwa kuwa nguzo ya familia na kuwalea watoto wote walionao wakati yeye akihangaika na masuala ya kitaifa.

Katika hatua nyingine, Abate Thadei Mhagama kutoka Abasia ya Hanga iliyoko Songea ambaye aliongoza ibada hiyo, aliwataka waamini wote nchini Tanzania wazidishe sala kwa kufunga na kuomba katika siku saba zilizobakia kabla ya uchaguzi mkuu kwa sababu hali ni tete. “Ninawaomba waumini wote tuzidishe sala ili kwanza pawe na amani na upendo na pia Mungu atuwezeshe kupata viongozi aliowandaa kwa maana ya Rais, Wabunge na Madiwani.”

“Sote ni mashahidi, tumeona kwenye mikutano kila mgombea akija sote tunajaa huko… hii ni kwa sababu hatujuia yupi ni yupi, ndiyo maana nasisistiza kuwa tumuombe Mungu atuletee yule ambaye amemuandaa,” aliongeza. Alisema kila mwananchi amesikia kwamba uchaguzi ukishafanyika awe tayari kupokea matokeo. “Tumeambiwa mara kadhaa tuwe tayari kukubali matokeo… kwa vile tunamuomba Mungu kwa bidii, itakuwa rahisi kukubali hayo matokeo kuliko kwa wale ambao wanaenda bila kuongozwa na Mungu,” alisema. “Litakuwa jambo jepesi kwetu kukubali matokeo kwani tutasema Mungu amemleta yule aliyemuandaa, yule ambaye tumekuwa tukimuomba atuletee,” alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza la Walei la Parokia hiyo, Bw. Arbogasti Warioba alisema kama kanisa wao wanamshukuru Mungu kwa ulinzi aliompatia Mhe. Pinda kwa kipindi chake chote cha Uwaziri Mkuu. “Sote tunatambua kuwa kazi ilikuwa ngumu, misafara ilikuwa ni mingi na wakati mwingine ya mwendo mkali lakini Mungu alikutetea na kukulinda hadi leo uko salama. Tunakushukuru pia kwa ushirikiano ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa madarakani na tunakuombea uendelee kuwa na uchaji wa Mungu katika maisha yako ya uraiani,”alisema Bw. Warioba.

Na Irene Bwire.

Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.