2015-10-19 09:45:00

Wakimbizi na wahamiaji ni chachu ya maendeleo, waheshimiwe!


Matatizo na changamoto za wakimbizi na wahamiaji hazina budi kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa mintarafu Malengo endelevu ya maendeleo ifikapo mwaka 2030 kama ilivyobainishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni. Ni mwaliko ambao umetolewa hivi karibuni na Monsinyo Gabriele Ferdinando Bentoglio, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum, wakati akichangia mada kwenye Jukwaa la wahamiaji na maendeleo, lililokuwa linafanyika huko Istanbul, Uturuki.

Jumuiya ya Kimataifa inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wakimbizi katika ustawi na ukuaji wa uchumi kwa nchi wahisani na mahali wanapotoka wakimbizi pamoja na wahamiaji hawa. Changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, inaanzisha mchakato wa uhamiaji salama, unaoratibiwa na kudhibitiwa kikamilifu, ili uweze kuambata sheria, kanuni na haki msingi za binadamu pamoja na kuthaminiwa utu wao kama binadamu bila kujali hali yao kama ni wakimbizi, wahamiaji au watu wasiokuwa na makazi maalum. Makundi yote haya ni msingi thabiti katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Monsinyo Bentoglio anakaza kusema, ni jambo lisilokubaliwa mbele ya macho ya Jumuiya ya Kimataifa kuona wahamiaji na wakimbizi wakiendelea kupoteza maisha kutokana na baadhi ya nchi zilizoendelea kutunga sheria na sera kali dhidi ya wahamiaji na wakimbizi. Haya ni makundi ambayo yamekuwa ni wahanga wa kampeni za wanasiasa wanaowania madaraka au vyombo vya habari vinavyotaka kutoa mwelekeo potofu kwa jamii kuhusiana na makundi haya, kuwa ni chanzo cha hatari katika usalama na mafungamano ya kijamii.

Nchi wanamotoka wakimbizi na wahamiaji zinapaswa kusaidiwa, ili kukabiliana na changamoto zinazopelekea watu kupata kishawishi cha kutaka kukimbia kutoka katika nchi zao za asili. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano; ugawaji na matumizi bora ya rasilimali ya dunia, ushirikiano wa kimataifa. Sera inayowaingiza wahamiaji na wakimbizi katika maisha na tamaduni za nchi hisani ni muhimu sana katika kukuza mchakato wa maendeleo endelevu na kwamba, hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Utu na  heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo. Hawa ni wajenzi wa madaraja ya tamaduni za watu kukutana; nguvu kazi katika uzalishaji na utoaji huduma; ni watu wenye mawazo na maoni tofauti yanayoweza kufanyiwa kazi kwa ustawi wa wengi. Lakini kwa bahati mbaya mara nyingi makundi haya ya watu yamekuwa ni chanzo cha ubaguzi, vurugu na kinzani kutokana na: utaifa na woga usiokuwa na mashiko!

Monsinyo Bentoglio anahitimisha mchango kwa kukaza kusema, wakati mwingine vijana walioandaliwa barabara wenye vyeti na taaluma zao wanalazimika kukimbia nchi za ona kusaliti majiundo yao ili kuziba pengo la kazi ngumu zinazokataliwa na watu wengi kutoka katika nchi zilizoendelea. Matokeo yake vijana kama wanajikuta wametumbukia au kutumbukizwa katika: biashara haramu ya binadamu na viungo; utumwa mamboleo pamoja na vitendo ambavyo vinadhalilisha utu na heshima yao kama binadamu.

Sheria, kanuni na taratibu ni muhimu sana katika kudhibiti wimbi la uhamiaji wa kiholela, ambao kwa sasa ni changamoto kubwa. Uwepo utaratibu mzuri wa kutumia nguvu kazi kutoka katika nchi changa zaidi, kwa ajili ya kusaidia mchakato wa ukuaji wa uchumi na utoaji huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.