2015-10-19 14:43:00

Papa aonya: haiwezekani kuwa mtumishi wa Mali na Mungu kwa wakati mmoja


Baba Mtakatifu Francisco anasema, Yesu hakatai mtu kuwa na mali, lakini anachokikataa ni mtu kushikamana mno na kuthamini fedha na utajiri kuliko watu wengine , kiasi cha kujitenga hata na wanafamilia au utajiri kuwa chanzo cha ugomvi na vita ndani ya familia au jamii. Papa alisema hilo wakati wa Ibada ya Misa ya asubuhi katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta, ndani ya Vatican.

Papa alionya dhidi ya kushikamana mno na utajiri, mshikamano wenye kuigeuza fedha na mali kuwa kama muungu wa kuabudiwa, roho ya uchoyo isiweza kugawana na wengine kilichopo. Papa alirejea maneno ya Yesu kwamba, ni vigumu kuwatumikia Mabwana wawili, mali na Mungu . Ni lazima kuchagua moja wapo, kuwa mtumishi wa Mungu au kuutumikia utajiri wa dunia. Na alifafanua kwamba, Yesu  hazunguzii juu ya mali tu  lakini anaulenga moyo wa mtu mwenyewe dhidi ya kuweka usalama maisha katika mali na kuifanya dini kama wakala tu wa bima. Na aliendelea kuzungumzia mapenzi kwa mali na  fedha yenye kusababisha hata  mgawanyiko ndani ya familia , kama Injili ilivyozungumzia juu urithi kati ya ndugu wawili.

Baba Mtakatifu Francisco ameeleza na kuonyesha kutambua jinsi mali katika familia nyingi huzua malumbano na chuki kiasi cha kuacha kusalimiana, kutengana na ugomvi mkubwa kati ya wanafamilia kutokana na urithi wa mali.

Papa amekumbusha hili na kuzitaka familia zote duniani, kwanza kabisa katika masuala ya urithi kuona jambo la kwanza muhimu ni familia kuendeleza zaidi  upendo kwa familia, upendo kwa watoto, ndugu, wazazi, bila kujali yaliyopo iwe fedha au mali.  Ni lazima kuwa na utambuzi kuwa mali na fedha ni mambo ya mpito, ni mambo ya kuharibika mara.  Yesu kwa uwazi alitutaka kuwa makini na mali , kukaa mbali na kila aina ya tamaa na uchoyo. Hata hivyo alionye, hii haina maana kwamba, tusiwe na bidii katika kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia mambo muhimu ya kutuhifadhi kimaisha. Hii haina maana kwamba tuwa watu wa kushinda Kanisani tukisali na kuwa  tegemezi wa watu wengine katika mahitaji ya maisha. La si hivyo Papa amesema, Yesu anataka mioyo yetu , isimezwe na kupenda fedha na mali kisia cha kumsahau Mungu. Kuwe na mshtuko wa moyo kwa yale yanayoongoza kwenye hatima mbaya ya kupenda mali zaidi kuliko Mungu. .

Katika Injili ya Siku , Yesu anatoa mfano wa  mtu mmoja tajiri, mwekezaji mzuri ambaye mwisho wa mavuno anaona amekamilika kwa utajiri tele. Yeye badala ya kufikiri jinsi atakavyo gawana faidi kubwa aliyopata na wafanyakazi wake, na  zaidi kuzifikiria  familia zao,  moyoni mwake,` anafikiria tu jinsi atakavyoongeza utajiri huo kwa kujenga ghala kubwa, lakini Mungu anamwambia naitaka roho yako sasa. Kumbe Mungu anampa sharti la utajiri ni kutoa sadaka, haja ya kujitoa kwa wengine kwa  upendo.  Papa alieleza na kurejea Mafundisho ya Yesu juu ya Heri, Heri wenye umaskini wa roho. Hiyo ndiyo  maana ya upendo mkubwa kwa Mungu kwamba, ni kujinasua na utajiri.

Papa alikamilisha kwa kumwomba Mungu  neema kuwa huru dhidi ya ibada ya sanamu ya fedha , na kujinasua na utajiri; Neema kwa kuangalia mbele hatima ya maisha, si katika utajiri lakini  katika upendo wake, ukarimu,  huruma yake na neema ya kutusaidia wengine kupitia utoaji wa  Zaka na michango mingi inayotakiwa kwa ajili ya misaada. Ni lazima kuwa na utambuzi kwamba hatupungukiwa na kitu kwa kuwa tukimwomba Baba Yetu hatunyimi kitu.








All the contents on this site are copyrighted ©.