2015-10-18 09:05:00

Sinodi ni matunda ya Kanisa linalotembea katika umoja!


Mshikamano, umoja na Ukatoliki wa Kanisa ni mambo msingi ambayo yameliwezesha Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini kuweza kutembea kwa pamoja, kusali na kutafakari kuhusu utume na maisha ya Kanisa la Kristo, huku likiwa  limeungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni hija ngumu yenye changamoto nyingi, lakini mwishoni inaonesha matunda ya furaha, amani na utulivu. Maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu wa Afrika, ilileta ari na mwamko wa pekee kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Maaskofu kutoka Afrika waliungana na Maaskofu wenzao kusali, kutafakari na kujadili kuhusu maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika katika hali ya umoja, udugu na upendo kwa kutambua kwamba, Kanisa ni familia ya Mungu inayowajibika. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa Jumamosi, tarehe 17 Oktoba 2015 na Askofu Mathieu Madega Lebouakehan, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon. Anasema, maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka wa kusikiliza na kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo.

Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipozindua maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kufaidika kwa kiasi kikubwa na mwono huu wa kinabii, kwa Maaskofu kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa la Kristo, kwa kusoma alama za nyakati. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanawawezesha Maaskofu na waamini walei kutembea kwa pamoja katika imani na matumaini.

Kwa upande wake Askofu mkuu Ricardo Ezzati Andrello wa Jimbo kuu la Santiago de Chile anasema, Sinodi ni hija ya pamoja inayoonesha umoja na usawa unaofumbatwa katika Sakramenti ya Ubatizo kwa kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, hali ambayo inajionesha katika Sinodi maalum, Mabaraza ya Maaskofu pamoja na Sinodi za majimbo katika Makanisa mahalia. Ni mahali pa kujadili na kutoa mbinu mkakati katika azma ya Uinjilishaji. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yameimarisha kwa namna ya pekee umoja na mshikamano wa Kanisa la kiulimwengu na Makanisa mahalia na kwa namna ya pekee Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini.

Sinodi za Maaskofu zimekuwa ni uwanja unaowajumuisha Wakleri, Waamini walei pamoja na mabingwa mbali mbali ili kujadili changamoto zinazolikabili Kanisa, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati za utekelezaji wake. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, mada ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu ni: Familia, Sakramenti za Kanisa, Majiundo makini ya Wakleri, Watawa na Waamini walei, Neno la Mungu na Uinjilishaji mpya. Mada zote hizi zimekuwa na umuhimu wa pekee katika kutengeneza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa la kiulimwengu na Makanisa mahalia. Sinodi ni fursa ya pekee inayowakutanisha Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hali inayoonesha umoja na mshikamano wa Kanisa chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.