2015-10-18 10:10:00

Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Papa Francisko Barani Afrika!


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Novemba 2015 anatarajiwa kutembelea Barani Afrika, ambako atapata fursa ya kukutana na kuzungumza na Familia ya Mungu, hususan: Wakleri, watawa na waamini walei; Viongozi wa kidini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo; Viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchini zao huko Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Kipaumbele cha kwanza ni kuwaimarisha waamini katika imani kwa Kristo na Kanisa lake; kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika pamoja na kuendelea kuwahimiza viongozi wa Serikali, Kisiasa na Kidiplomasia kujikita katika mchakato wa haki, amani, mafao ya wengi na upatanisho wa kweli kama vigezo muhimu katika ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Barani Afrika. Maskini, vijana na wakimbizi watakuwa na upendeleo wa pekee wakati wa hija ya Baba Mtakatifu Barani Afrika atakapokuwa anatembelea: Nairobi, Entebe, Munyonyo, Namugongo, Kampala, Nalukolongo na Bangui.

Ratiba rasmi iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba, tarehe 25 Novemba 2015,majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko ataondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Fumicino na kuwasili saa 11: 45 jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi. Baada ya kukaribishwa rasmi nchini Kenya, atakwenda kumtembelea Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na hapo atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao Kenya.

Alhamisi, tarehe 26 Novemba 2015, Baba Mtakatifu ataianza siku kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na madhehebu ya Kikristo nchini Kenya, kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Kenya. Baadaye atakwenda kwenye Uwanja wa Chuo kikuu cha Nairobi ambako ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na jioni atakutana na watawa na majandokasisi kutoka Kenya kwenye uwanja wa michezo wa shule ya St. Mary, Nairobi. Baba Mtakatifu atahitimisha siku ya pili ya hija yake nchini Kenya kwa kutembelea Ofisi za Umoja wa Mataifa ziliko mjini Nairobi.

Ijumaa, tarehe 27 Novemba 2015, asubuhi na mapema, Baba Mtakatifu Francisko atawatembelea na kuzungumza na watu wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kitongoji cha Kangemi, kilichoko Jijini Nairobi, kwani maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu atakutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Kenya katika Uwanja wa michezo wa Kasarani.

Kabla ya kuondoka kuelekea Entebe, Uganda, Baba Mtakatifu akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwenye chumba cha watu maarufu uwanjani hapo. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Entebe majira ya jioni.

Jumamosi, tarehe 28 Novemba 2015, Baba Mtakatifu ataianza siku yake ya pili nchini Uganda kwa kutembelea Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda kutoka katika Kanisa Anglikani na baadaye atatembelea Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda yaliyoko Namgongo na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Atakutana na vijana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kampala, Uganda, atatembelea nyumba ya huduma ya upendo iliyoko Nalukolongo na baadaye jioni atakutana na Wakleri, watawa na majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Kampala, Uganda.

Jumapili, tarehe 29 Novemba 2015, Baba Mtakatifu ataondoka nchini Uganda kuelekea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kuwasili asubuhi majira ya saa 4:00 kwa saa za Afrika ya Kati. Hapo atapokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa “M’Poko, Bangui kwa heshima zote za kitaifa. Baba Mtakatifu atazungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Atatembelea kambi ya wakimbizi, atazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati pamoja na kuzungumza na viongozi wa Madhehebu ya Kikristo nchini humo, tukio litakalofanyika kwenye Kitivo cha Kitaalimungu cha Makanisa ya Kiinjili Bangui. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atawaungamisha baadhi ya vijana watakaokuwa wameandaliwa pamoja na kuzindua mkesha wa sala kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Bangui.

Jumatatu, tarehe 30 Novemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko ataianza siku yake kwa kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya waamini wa dini ya Kiislam kwenye Msikiti mkuu wa Koudoukou, mjini Bangui, baadaye, atakwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa Barthèlèmy Boganda. Majira ya mchana, Baba Mtakatifu atakuwa anatua nanga ya hija yake ya kitume Barani Afrika, tayari kurejea mjini Vatican, kuendelea na maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwasili usiku kwenye Uwanja wa Ciampino, Mjini Roma.

Kama kawaida ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yanayojiri wakati wa hija hii, lakini ukiwa na haraka zako, usikose kutupia jicho kwenye mtandao wa Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.