2015-10-18 13:37:00

Kataeni kishawishi cha chuki na hali ya kulipizana kisasi! Jengeni amani!


Mara baada ya Maadhimisho ya Misa Takatifu, Jumapili tarehe 18 Oktoba 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini vatican, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na machafuko na kinzani za kijamii zinazoendelea kupamba moto huko Nchi Takatifu.

Anasema, huu ni wakati ambao unahitaji kwa namna ya pekee kabisa: ujasiri na nguvu ya ndani, ili kukataa kishawishi cha chuki na hali ya kutaka kulipiza kisasi na badala yake, kujielekeza katika ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuimarisha nguvu na utashi wa viongozi wa Serikali na wananchi, kuwa na ujasiri wa kuondokana na matumizi ya nguvu kwa kujikita katika matendo mema. Amani na utulivu katika Nchi Takatifu ni muhimu sana huko Mashariki ya Kati, changamoto kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya mafao ya binadamu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewasalimia wajumbe wote waliofika kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kushiriki katika Ibada ya kuwatangaza watakatifu wapya, watu ambao wameonesha mfano bora wa kuigwa katika uongozi unaojikita katika huduma kwa vijana; maskini na wagonjwa bila kusahau ustawi na maendeleo ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.