2015-10-17 08:00:00

Injili ya familia na changamoto zake!


Mababa wa Sinodi katika tafakari zao wanasema, maandalizi ya wanandoa watarajiwa iwe ni safari ya maisha ya imani inayojikita katika Mafundisho tanzu ya Kanisa, ushuhuda na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; haki, upendo na huruma ya Mungu. Waamini wawe na mwono chanya kuhusu tendo la ndoa kwa kuzingatia: uzuri, utakatifu, dhamana na wajibu wake kwani, kwa njia ya tendo la ndoa mwanaume na mwanamke wanashiriki katika kazi ya uumbaji na malezi.

Tendo la ndoa liheshimiwe na kamwe lisipigwe “danadana” kwa kupokwa na wafanyabiasha wanaotaka kuuza kondom; kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa biashara ya ngono; mambo yanayokumbatia utamaduni wa kifo, hatari kwa Injili ya familia. Waamini waelimishwe kutambua na kuthamini useja kama sehemu ya mtindo wa maisha si tu kwa watawa na mapadre, bali hata kwa wanandoa na familia. Uaminifu na udumifu ni mambo msingi sana katika maisha ya ndoa na familia na kwamba, “chocho”  au “nyumba ndogo” ni chanzo cha majanga mengi ndani ya familia.

Watoto wana haki zao msingi, zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa na wazazi pamoja na jamii husika. Waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu hasa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; kwa familia maskini na zisizokuwa na uwezo mkubwa wa kujikimu katika maisha. Watoto wakilelewa vyema wanaweza kuwa ni wadau wakuu katika azma ya Uinjilishaji mpya, wajengewe ari na moyo wa kimissionari tangu wakiwa na umri mdogo.

Mababa wa Sinodi wameendelea kuhimiza umuhimu wa wazazi na walezi kujikita katika upendo mkamilifu unaoambata uwajibikaji wa dhati, kwa kuambata Injili ya maisha, ili kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo kama anavyokazia Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kitume Maisha ya mwanadamu “Humanae Vitae. Wanandoa waoneshane upendo wa dhati unaofumbatwa katika sadaka na majitoleo ya kweli kati yao. Wanandoa waelimishwe zaidi na zaidi uzuri, utakatifu na wajibu wa tendo la ndoa katika maisha ya kifamilia, kama sehemu ya majiundo kamili ya Kikristo.

Utoaji wa mimba na vizuia mimba ni mambo ambayo yanakumbatia utamaduni wa kifo na kujikita katika biashara na wala si kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanandoa wenyewe. Wanafamilia wapewe elimu ya kutosha kuhusu mada hizi kwa kusaidiwa na wataalamu wanaoaminika, ili kuliwezesha Kanisa kuwa ni mahali pa rejea katika masuala ya maadili na utu wema katika masuala ya uzazi. Familia zenye mgogoro wa imani zisikilizwe, ziheshimiwe na kuthaminiwa, ili kamwe zisijisikie kuwa pweke.

Makanisa mahalia yaunde vituo vya kusikiliza na kushauriana kuhusu migogoro ya maisha ya ndoa na familia, ili kuzuia, kuganga na kuponya myumbo wa maadili, imani na matumaini katika familia. Viongozi wa Kanisa wawe ni wahudumu na wasamaria wema kwa familia. Wanandoa wakuze na kudumisha mahusiano mema na jirani zao, jamii na mazingira yanayowazunguka, ili kupata ekolojia kamilifu katika maisha ya kifamilia. Hii inatokana na ukweli kwamba, familia ni waathirika wa kwanza kunapotokea athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa au yanapotokea majanga asilia na maafa.

Kwa wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuoana watambue kwamba, Sakramenti ya Ndoa ni dumifu na kwamba wanapaswa kutambua ukweli huu na kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuimarisha uelewa huu, kabla ya kuruhusiwa kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Hapa kuna haja ya kuwa na wachungaji wanaojikita katika katekesi makini inayoambata Injili ya Kristo, tayari kuwasaidia wanafamilia hawa kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao, ili kukumbatia huruma ya Mungu. Huu ndio mwelekeo unaopaswa kutumiwa na Makanisa mahali katika kuwasaidia wanandoa kuanza safari ya toba na wongofu badala ya kukazia sheria na haki peke yake.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, Ndoa ni umoja kamili na wa kudumu kati ya bwana na bibi; usioweza kuvunjika au kuvunjwa; upendo huu unawashirikisha mume na mke kwa ajili ya mafao yao wenyewe, kwa ajili ya kupata watoto na kuwalea kikamilifu. Mchakato wa kuwaruhusu wanandoa waliotalakiana kupokea Ekaristi Takatifu maana yake ni kubadili Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na nidhamu ya Kanisa. Ili safari ya toba na wongofu wa ndani, iweze kuwa kamili, kuna haja kabisa ya kutubu na kudhamiria kutorudia tena dhambi hii, kwa kukishinda kishawishi cha kuzini.

Mada hii inapaswa kufanyiwa kazi tena na Mababa wa Sinodi, pengine kwa kuunda Tume maalum itakayokuwa chini ya usimamizi na uongozi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa. Huruma ya Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani inaunganisha mbingu na dunia na kutoa mwanga katika mapito ya historia ya mwamini; kwa kuzingatia ukweli na haki. Changamoto ya wanafamilia waliotalakiana inapaswa kuwa na mwono mpana zaidi katika masuala ya kitaamungu, ili kutokuwa ni kikwazo kwa wanandoa ambao wamekuwa waaminifu katika kifungo cha ndoa, maadili na kanuni za Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanasema, kuna vipigo vinavyoendelea ndani ya familia, wanawake wakiwa ni waathirika wakubwa, lakini pia kuna kundi la wanaume wanaokung’utwa na wake zao, kiasi cha kusikitisha. Mambo haya hayazungumzwi sana hadharani kwani ni mambo ya ndani ya familia, lakini huu ndio ukweli wa mambo, huu ndio utamaduni wa ukimya katika ndoa. Wazee na walemavu waheshimiwe na kuthaminiwa na kamwe wasitengwe na kubaguliwa, kwani watakufa katika upweke na majonzi makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.