2015-10-16 07:21:00

Sinodi za Maaskofu ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican


Mama Kanisa tarehe 17 Oktoba 2015 anaadhimisha Jubilei ya miaka hamsini tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican  walipoamua Kanisa liadhimishe Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya kutafakari maisha, utume na changamoto zinazolikabili Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, ili Maaskofu wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro waweze kutoa ufumbuzi wa changamoto hizi kwa wakati muafaka.

Mwenyeheri Paulo VI wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu alikazia umuhimu wa Mababa wa Sinodi kuimarisha: imani, mapendo na shughuli za kichungaji kwa ajili ya Makanaisa mahalia, Mashirika ya Kitawa na Kanisa la kiulimwengu. Sinodi iwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa; chombo cha ushauri unaotokana na mchango wa familia ya Mungu, ili kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya Kanisa la Kristo.

Sinodi ya Maaskofu kwa kiasi kikubwa ni Baraza la ushauri linalojikita pia katika mchakato wa Kiekumene, kwa kuwapatia wajumbe fursa ya kushirikisha karama na mawazo yao kadiri Roho Mtakatifu anavyowawezesha. Ni wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wenye hadhi na mamlaka kamili, ambao mawazo, tafakari na mchango wao wakati wa maadhimisho ya Sinodi unapaswa kujikita katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa lake na kwamba, wao wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda amini na wachungaji makini wa Watu wa Mungu. Wasaidiwe na mabingwa na wataalam mbali mbali ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Wawakilishi wa wakuu wa Mashirika wakiungana pamoja na wasaidizi wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro walishirikishane uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa.

Tangu wakati huo, Mwenyeheri Paulo VI alikwisha sema kwamba, inawezekana kabisa kwamba, Mababa wa Sinodi walioalikwa wakashindwa kuhudhuria katika maadhimisho ua Sinodi kutokana na sababu mbali mbali, hata pengine kunyimwa kibali na Serikali husika, lakini bado wataendelea kuoneshwa mshikamano wao wa dhati. Hata leo hii bado kuna baadhi ya wajumbe wa Sinodi kutokana na sababu mbali mbali wanaweza kushindwa kuhudhuria vikao vya Sinodi.

Mwenyeheri Paulo VI anasema, vikwazo hivi vinaweza kusababishwa na ukosefu wa haki, amani na uhuru wa kuabudu katika baadhi ya nchi; dhuluma na nyanyaso dhidi ya Kanisa Katoliki. Yote haya ni mambo yanayokwamisha uhuru wa kidini, jambo msingi katika utekelezaji wa haki za binadamu. Kanisa linayapongeza na kuyashukuru mataifa ambayo yanajikita katika uhuru wa kuabudu na kutoa fursa kwa Kanisa kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya watu katika nchi hizo pasi na ubaguzi. Lakini pia Kanisa linaonesha mshikamano wake wa dhati na waamini ambao wanaendelea kuiungama na kuishuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika hali ya ukimya pasi na makuu. Wote hawa wanapaswa kukumbukwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu.

Mwenyeheri Paulo wa VI analitaka Kanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekuemene ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuwaalika wajumbe kutoka katika Makanisa mbali mbali ya Kikristo kushiriki katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, ili kuweza kutembea pamoja hata katika maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa nyakati hizi. Ushirikiano na Makanisa mengine ni fursa ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene, ili kuendeleza Mapokeo ya Kanisa sanjari na kukoleza umoja na mshikamano.

Ufunguzi wa Sinodi ya Maaskofu anakaza kusema Papa Paulo VI hauna budi kuelekezwa kwa Familia yote ya Mungu na hususan kwa waamini wa Makanisa ambayo bado hayana umoja kamili na Kanisa Katoliki, lakini yanaunganishwa pamoja na vifungo mbali mbali vya maisha ya kiroho katika imani, matumaini na mapendo. Sinodi za Maaskofu ziwe ni chachu ya majadiliano ya kiekumene, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo.

Mwenyeheri Paulo VI anasema, wakati wa Maadhimisho ya Sinodi, Mababa wa Sinodi wakumbuke daima kusali kwa ajili ya kuombea: haki na amani duniani. Mababa wa Sinodi watambue kwamba, bado kuna watu wanateseka kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kidini sehemu mbali mbali za dunia. Ni wajibu wa Kanisa kumwomba Yesu Kristo Mfalme wa amani, ili aweze kuwajalia walimwengu amani ya kudumu. Kanisa liendelee kuwa ni chombo cha amani, kwa kusaidia kuunda dhamiri nyofu, kwa kujikita katika misingi ya haki na uhuru kamili.

Ni wajibu wa Kanisa kuwaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha amani inatawala kwa kudhibiti biashara ya silaha ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa ya watu wengi wasiokuwa na hatia. Jumuiya ya Kimataifa iwe mstari wa mbele katika kukoleza majadiliano yanayopania kusitisha vita na migogoro sehemu mbali mbali za dunia. Familia ya Mungu ioneshe mshikamano wa upendo na wale wote wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kinzani mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.