Ole wenu, enyi wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazua. Kwa maneno haya Yesu anaonesha ukali kwa wanasheia ambao wamekuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa amri ya upendo kwa jirani, hali ambayo inaonesha kishawishi cha kutaka kudhibiti kazi ya wokovu. Waamini watambue kwamba, wokovu ni zawadi ya bure kabisa ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia binadamu wote pasi na kinyongo. Huu ndio msimamo unaokaziwa pia katika Mafundisho ya Mtakatifu Paulo, mwalimu wa mataifa katika nyaraka zake mbali mbali.
Yesu Kristo, Mwana wa Mungu alikuja duniani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumkirimia upendo na maisha ya uzima wa milele, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Huu ni upendo usiokuwa na mipaka; mafundisho ambayo waamini wengi wamezoea kuyasikia, lakini pengine, hawayapatii uzito wa kutosha katika maisha yao.
Wanasheria wamekumbatia ufunguo wa maarifa kuhusu wokovu na wao wenyewe washindwa kuingia ndani, kwa kudhani kwamba, kwa njia ya kurudia rudia Amri za Mungu wangeweza kupata furaha ya maisha ya uzima wa milele, dhana ambayo, ilidhohofisha mwelekeo mpana wa upendo wa Mungu kwa waja wake. Yesu anakaza kusema, upendo wa Mungu hauna mipaka wala haubagui mtu awaye yote!
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 15 Oktoba 2015, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Muhtasari wa Amri kuu ni upendo kwa Mungu na jirani, unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini na wote wenye mapenzi mema. Upendo ni chemchemi na kilele cha huruma ya Mungu kwa binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, mwanamke wa shoka ambaye alibahatika kuwa na neema na mang’amuzi wa upendo wa Mungu; akahukumiwa na wanasheria wa nyakati zake, akateswa na kunyanyaswa, kama walivyo watakatifu wengi ndani ya Kanisa, kati ya Mtakatifu Yohane d’Arco. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kusimama kidete kukumbatia huku wakiambata wokovu unaobubujika kutoka katika upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, ili kweli kuendelea kujikita katika upendo unaofumbata huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |