2015-10-15 14:32:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 89 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2015


Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 89 ya Kimissionari Ulimwenguni hapo tarehe 18 Oktoba 2015, maadhimisho ambayo yanakwenda sanjari na Mwaka wa Watawa Duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu, anaonesha mahusiano makubwa yaliyopo kati ya maisha ya kitawa na utume wa Kanisa wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Anawachangamotisha vijana kujisadaka kwa ajili ya kushiriki katika azma ya Uinjilishaji wa watu kwa kujikita katika malezi makini, utamadunisho na ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayosimikwa katika huduma ya mapendo. Ili kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji, watawa wanahimizwa na Baba Mtakatifu kushirikiana na waamini walei, ili kuwasaidia kutekeleza dhamana waliyoipokea wakati wa Ubatizo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna uhusiano wa pekee kati ya maisha ya kitawa na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika ufuasi kwa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha ya kitawa. Watawa wanaalikwa kwa namna ya pekee kubeba vyema Misalaba yao, tayari kumfuasa Kristo, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma upendo kwa Watu wa Mungu, kwani uwepo wa Kristo unachapa ya kimissionari na kwamba, hii pia ni sehemu ya maisha ya kitawa na vinasaba vyake. Huu ni mwaliko kwa watawa kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu anayewaita na kuwatuma, ili kumwambata Kristo, tayari kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji.

Utume anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha upendo kwa Kristo na Watu wa Mungu, kwa kutambua ukuu wa upendo wake unaowategemeza, kwani upendo huu unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, ni upendo kwa ajili ya binadamu wote, upendo unaopania kuonesha ule ukaribu wa Yesu kwa wale wote wanaomtafuta Mungu kwa moyo mnyofu. Kanisa linatambua changamoto zilizopo katika Uinjilishaji, mwaliko kwa waamini, lakini kwa namna ya pekee, watawa kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao, tayari kujisadaka kwa kuwaendea wale wote ambao hawajabahatika kusikiliza Injili ya furaha.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita, ilikuwa ni chachu kubwa ya kuibuka kwa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume; yaliyoamsha ari na kuleta mwamko mpya wa shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia; na huo ukawa ni mwanzo wa utamadunisho wa maisha ya kitawa, kwa kumweka Kristo Yesu kuwa ni kiini cha mchakato wa Uinjilishaji.

Watawa wanahamasishwa kuwa makini katika maisha na utume wao wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza na kuendelea kujikita katika malezi bora na makini, tayari kuwafunda watawa wa baadaye kuwa kweli ni wahudumu makini wa Injili ya Kristo. Walezi wanapaswa kuwasaidia walelewa katika ukweli, uwazi na umakini wito wa maisha ya kitawa, ili kuwasaidia vijana wajasiri kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Utawa ni sadaka ya upendo kwa ajili ya huduma ya Injili na kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa watawa kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, Uinjilishaji na Utamadunisho ni kati ya changamoto zinazoendelea kuliandama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Watawa wanaalikwa kutambua, kuheshimu na kuthamini mila na tamaduni njema zinazoweza kuwasaidia kumtambua Mwenyezi Mungu na kuambata Injili ya Yesu ambayo kimsingi ni mwanga kwa tamaduni mbali mbali na chachu ya mageuzi ya kitamaduni. Walengwa wakuu wa Uinjilishaji ni maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa ndio wanaopaswa kutangaziwa uwepo wa Ufalme wa Mungu na kwamba, imani na maskini ni chanda na pete!

Watawa kwa njia ya nadhiri ya ufukara wanataka kumfuasa na kumuiga Yesu Kristo aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, akajinyenyekeza, ili aweze kuwa ni rafiki ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; mwaliko kwa watawa kuwa ni vyombo vya Injili ya furaha na kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Kwa njia ya nadhiri ya ufukara, watawa wanahamasishwa kuwashirikisha waamini walei ile mbegu ya upendo kwa njia ya huduma, kwa kushirikiana na waamini walei wanaotolea ushuhuda wa neema ya Sakramenti ya Ubatizo. Taasisi za kitawa ni mahali muafaka pa kuwakarimu na kuwasaidia waamini walei: kiutu, kiroho na kitume.

Watawa wawe na taasisi anasema Baba Mtakatifu zinazoonesha huduma na ushuhuda wa kimissionari, huku wakijikita katika umoja kama anavyo agiza Yesu mwenyewe kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unahitaji kuambata karama mbali mbali ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya furaha, uhuru na wokovu kwa watu wote. Ni Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha, unaopaswa kwa namna ya pekee kutolewa na mihimili yote ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 89 ya Kimissionari Duniani kwa kukumbusha kwamba, kila Mkristo anapaswa kuishi kikamilifu dhamana yake ya Ubatizo kadiri ya hali na wito wake pamoja na kuendelea kushirikiana na watawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.