2015-10-15 11:53:00

Injili ya Familia ni kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu


Mababa wa Sinodi katika taarifa yao kutoka kwenye makundi madogo madogo wanasema Injili ya familia ni kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya familia, inayojikita katika Neno la Mungu, mwaliko na changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kukumbatia maisha ya ndoa na familia, pamoja na familia kuendelea kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa unaojikita katika mapendo thabiti na dumifu.

Kuna uhusiano wa pekee kati ya Sinodi na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwamba, familia zinahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Mababa wa Sinodi wanasema, mwanamke hapigwi kwa rungu na  mateke, bali wa busu la upendo na msamaha; familia zijitahidi kushikamana!

Mababa wa Sinodi wanasema katika tafakari zao kwamba, sehemu ya pili ya Hati ya kutendea kazi, Instrumentum Laboris inajikita katika Injili ya familia, kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia. Ni sehemu inayofafanua kwa kina na mapana Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa na familia. Mababa wa Sinodi wanasema, hii ni sehemu ambayo inapaswa kupewa uzito wa pekee katika tafakari na majadiliano ya Mababa wa Sinodi sanjari na kufanya marekebisho, ili iweze kuwa rahisi, wazi na kueleweka na waamini wengi zaidi, kwa kuonesha mvuto na mguso katika maisha na utume wa ndoa na familia unaojikita katika Injili ya familia inayoambata matumaini, pasi na kukata tamaa licha ya matatizo na changamoto zinazojitokeza katika uhalisia wa maisha.

Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kufanya rejea nyingi zaidi kwa Neno la Mungu kuhusiana na maisha ya ndoa na familia, kielelezo cha Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji kwa watu wa nyakati hizi. Vijana wanahamasishwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuambata Sakramenti ya Ndoa, wakitambua kwamba, kile ambacho kimeunganishwa na Mungu, mwanadamu hana ruhusa ya kukitengua.

Vijana waoneshwe ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kamwe wasikatishwe tamaa kwa kisingizio kwamba, vijana wa kizazi kipya hawana “ubavu” wa kuambata Sakramenti ya Ndoa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu mintarafu tamaduni, hali ya uchumi na gharama ya maisha, mambo ambayo yanawaathiri vijana katika kufanya maamuzi ya muda mrefu.

Ni wajibu na dhamana ya Mama Kanisa na wanandoa kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kuwa ni jambo ambalo linawezekana. Sakramenti ya Ndoa inajikita katika upendo kamili pasi na shurutu na kwamba, hili ni agano la kudumu, hadi kifo kitakapowatenganisha. Ni mahali pa kushuhudia neema na rehema zinazotolewa na Mwenyezi Mungu katika maisha ya ndoa na familia, kwa kukasidiana, kutakatifuzana kukamilishana. Ndoa na wito unaohitaji maandalizi yanayojikita katika maamuzi mazito ya maisha, tayari kujenga umoja na mapendo katika familia. Kuna uhusiano mkubwa kati ya familia na wito wa maisha ya kitawa; watawa ni matunda ya familia, Kanisa linawapongeza wakati huu wanapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, kuna uhusiano mkubwa kati ya Sinodi ya familia na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza wanandoa kuonja na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Hapa kuna haja ya kuendelea kupembua kwa kina na mapana kuhusu Sakramenti ya Ndoa; Haki, Upendo na huruma ya Mungu; mambo msingi katika utume wa Kanisa kwa familia, hususan familia zinazoogelea katika shida na mtikisiko wa imani katika maisha ya ndoa. Huruma ya Mungu iwaguse, iponye na kuganga madonda na machungu ya familia.

Mababa wa Sinodi wanasema família na Uinjilishaji ni sawa na chanda na pete ni mambio yanayotegemeana na kukamilishana. Familia zinahamasishwa kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani; wazazi na walezi ni Makatekista wa kwanza wenye dhamana ya kurithisha imani, maadili na utu wema kwa watoto wao. Wazazi wajenge na kudumisha moyo wa sala, sadaka na matendo ya huruma, kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha mshikamano na mafungamano ya kifamilia.

Mababa wa Sinodi wanasikitishwa na vipigo pamoja na ukatili wanaofanywa wanawake majumbani, lakini wengine pia wanasema, kuna wanaume wanaopata mkong’oto lakini wanaona aibu kusema ni mambo ambayo yanadhalilisha uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na família. Wanafamilia wanaokabiliana na magumu kama haya wasaidiwe, ili kuonja furaha ya maisha ya ndoa! Ni wajibu wa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, yanasaidia kuenzi na kudumisha shule na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Makanisa mahalia, ili kukazia uzuri na utakatifu w andoa.

Wanandoa wafundwe kuhusu Sakramenti ya Ndoa; vyama vya kitume na Parokia ziwe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Familia. Mababa wa Sinodi wanawaomba Maaskofu mahalia na wataalam wa Sheria za Kanisa kutoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu Waraka binafsi wa Baba Mtakatifu Francisko “Mitis Iudex” inayoelezea mchakato mfupi wa kubatilisha Ndoa zenye utata. Maaskofu waangalie kwa jicho la upendo na huruma hali halisi na pale wanapojiridhisha kwamba, hapa imeshindikana waweelezee wahusika kuhusu uwezekano wa kutengua ndoa tata!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.