2015-10-14 10:40:00

Walitaka kuchafua mazingira ya Sinodi ya Maaskofu!


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yanaendelea katika hali ya amani, utulivu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Barua inayosadikiwa kuandikwa na Makardinali kumi na watatu na kuchapishwa na baadhi ya vyombo vya habari, haina ukweli wa maudhui yaliyoandikwa na kwamba, Makardinali wanaohusishwa na barua hii wamekana kushiriki katika kuandika barua hii. Ni barua ambayo ilipania kuchafua mazingira ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu inayoendelea hapa mjini Vatican.

Hayo yamebainishwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 13 Oktoba 2015 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, ili kujuza kwa ufupi yale yanayoendelea kujiri katika maadhimisho ya Sinodi. Kimsingi, mtindo wa maadhimisho ya Sinodi ni mpya na ufafanuzi huu ulikwishatolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ufunguzi wa Sinodi na kupembuliwa zaidi na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu.

Padre Lombardi anakaza kusema, Kardinali Wilfrid Fox Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini amekanusha madai kwamba, alikuwa anatia shaka maamuzi ya Baba Mtakatifu Francisko kuunda Tume ya Wajumbe 10 kutoka katika Sinodi ili kuandika Ujumbe wa Mababa wa Sinodi mara baada ya maadhimisho ya Sinodi na badala yake alisema Baba Mtakatifu ana dhamana na wajibu wa kusimamia maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, kwa kufanya uteuzi kadiri anavyoona inafaa.

Abate Jeremiah Schròder, Mkuu wa Shirika la Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia, ambaye anawawakilisha wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume amezungumzia kuhusu uhusiano mkubwa uliopo kati ya familia, wito na maisha ya kitawa. Mwelekeo wa sasa unaonesha kwamba, watawa wengi si wale wanaotoka katika familia imara za Kikristo, bali ni vijana ambao wamepata mang’amuzi na wito wao katika hija ya maisha; wakajikita katika katekesi makini, kiasi cha kujikuta wanakuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kuna mabadiliko makubwa katika msingi wa maisha ya kitawa na kazi za kitume, changamoto ya kuwa na malezi makini na endelevu kwa watawa, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao .

Akigusia kuhusu wazo la Kanisa kuwa na Mashemasi wanawake, Abate Schròder anakiri kwamba, ameguswa na wazo hili kutoka kwa baadhi ya Mababa wa Sinodi ya familia, kwamba ni jambo linalowezekana hata kwa Kanisa Katoliki, lakini hadi sasa, mambo yatabaki kama yalivyo kwani ni wazo ambalo halijaungwa mkono na Mababa wengi wa Sinodi.

Mama Thèrese Nyirabukeye, mjumbe wa Sinodi kutoka Rwanda anakiri kwamba, mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda kunako mwaka 1994 yalisababisha majanga makubwa kwa ustawi na maendeleo ya familia nyingi nchini Rwanda. Familia kwa sasa inachukua kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa, kwa njia ya ushuhuda wa misingi ya haki, amani na mapendo. Na Mama Moira McQueen anawapongeza Mababa wa Sinodi kwa kuwasikiliza kwa makini wanapochangia mawazo na tafakari zao wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inayoendelea hapa mjini Vatican. Hiki ni kielelezo cha mchakato wa demokrasia, upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.