2015-10-14 11:12:00

Mwalimu Julius Nyerere: Jamani uongozi ni huduma!


Familia ya Mungu nchini Tanzania kila mwaka ifikapo tarehe 14 Oktoba wanafanya kumbu kumbu ya Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipofariki dunia nchini Uingereza kunako mwaka 1999. Maadhimisho ya Mwaka huu yana umuhimu wa pekee sana, wakati huu watanzania wapoendelea kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, huku wagombea uongozi mbali mbali wakijinadi majukwaani. Jambo ambalo linaendelea kuwasikitisha wengi ni kampeni za matusi na kejeli badala ya kutangaza sera na mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Askofu mkuu Josephat Lous Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, anamkumbuka Mwaliku Nyerere kuwa ni kiongozi ambaye aliijali Tanzania na wananchi wake, akajisadaka kimasomaso kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, kwani kwake uongozi ilikuwa ni huduma makini.

Leo hii viongozi wa Serikali, Kisiasa na Kidini wanahamasishwa kusimama kidete kushughulikia ustawi na maendeleo ya watanzania, kwani wana wajibu mkubwa mbele ya Mungu. Wataulizwa ni kwa namna gani viongozi hawa wamejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mustakabali wa Tanzania katika masuala ya: haki, amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya watanzania, kwa kuzingatia utu na heshima ya kila mtanzania.

Askofu mkuu Lebulu anakaza kusema, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa taifa la Tanzania ataendelea kukumbukwa na wengi ndani na nje ya Tanzania kwa kusimamia misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu bila ubaguzi. Hata Tanzania ya wakati huu, inawahitaji watu kama hawa wanaoweza kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya wengi, badala ya kujikita katika uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka. Uongozi ni huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.