2015-10-14 15:19:00

Mwalimu Julius Nyerere ataendelea kukumbukwa na wengi!


Mheshimiwa Padre Chesco Msaga, Makamu Askofu Jimbo kuu la Dodoma amewataka watanzania kushiriki uchaguzi mkuu na kuwachagua viongozi wanaowataka kwa utulivu na amani kwa kufuata misingi aliyoiacha Baba wa taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere. Msaga alitoa rai hiyo wakati akitoa mahubiri kwenye ibada maalumu ya kumuombea hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Kamabalage Nyerere, iliyofanyika katika viwanja vya Kumbukumbu ya Nyerere mjini Dodoma, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2015.

Padre Chesco Msaga ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kanda ya Tanzania, C.PP.S, alisema kuwa watanzania hawana budi kuishi kutokana na misingi aliyoicha Mwalimu Nyerere ambayo ni amani, umoja na mashikamano wa kitaifa ambazo ndizo tunu kubwa kwa taifa la Tanzania. Alisema kuwa katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 25  Oktoba, 2015 watanzania wanatakiwa kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi wanayemtaka bila kuharibu amani na mshikamano aliouenzi Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake.

“Tusiharibu kabisa misingi aliyoweka Baba wa taifa kwa kutaka madaraka kwa fujo au kufanya fujo ili kuweza kujipatia sifa za kisiasa hivyo basi niwasihi kuhakikisha amani utulivu na mashikamano aliyoiweka Baba wa taifa tunailinda katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kushiriki katika kupiga kura bila ya kumbuguzi mtu” alisema Padre Msaga. Aidha alisema kuwa watanzania wanatakiwa kuiga mambo mengi aliyokuwa akiyafanya Baba wa taifa ikiwa ni pamoja na kutokuwa na tabia ya kujilimbikizia mali kama ilivyo kwa baadi ya watu. “Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hakuwa na tabia ya kujilimbikizia mali kwani kila alichokipata alipenda watanzania wote wakipate bila kubagua kabila au dini hali iliyotufanya tuwe wamoja hadi leo hii” alisema.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa, akitoa salamu za mkoa katika ibada hiyo alisema kuwa watanzania wataendelea kumkumbuka Baba wa taifa kwa mambo mengi ambayo aliyafanya wakati wa uhai wake kwa kuwafanya wawe wamoja.“Leo tunadhimisha kumbu kumbu ya Kifo cha Baba yetu wa Taifa Mwalimu Nyerere lakini tutaendelea kumkumbuka kwa mambo mengi aliyotufanyia wakati wa uhai wake ambayo na sisi tunatakiwa kuyaishi ili kuweza kendeleza amani na mshikamano wa kitaifa  aliouacha” alisema Gallawa. Katika ibada viongozi wengine walioshiriki ni Spika wa Bunge Anna Makinda, Waziri wa habari utamaduni na Michezo Fenela Mukangala, Katibu Mkuu Tamisemi Jumanne Sagini pamoja na makatibu tawala na wakuu wa Wilaya mbalimbali.

Na mwandishi maalum.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.