2015-10-13 08:59:00

Kuzeni ari na moyo wa kimissionari, ili kutangaza Injili ya Furaha!


Zaidi ya wadau elfu mbili na mia mbili wa Uinjilishaji nchini Argentina, kwa muda wa siku tatu, kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 12 Oktoba, 2015 wamekuwa wakikisanyika kwenye mji wa Santiago del Estero, ili kushiriki katika kongamano la nne la kimissionari kitaifa, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Utume ni mtindo wa maisha”. Kongamano hili limehitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa “Quimsa” huko Santiago del Estero sanjari na kuwatuma wamissionari wapya kutoka kimasomaso ili kuwatangazia Watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika ushuhuda wa maisha. Itakumbukwa kwamba, kongamano la kwanza la kimissionari kitaifa lilifanyika nchini Argentina kunako mwaka 1990.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anawakumbusha wajumbe kwamba, wanayo dhamana ya kuwashirikisha wengine kile ambacho wamekishuhudia kwa kuona na kusikia, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu na kwamba, waendelee kutumainia na kujiaminisha katika nguvu inayobubujika kutoka kwa Yesu, ili kuwaimarisha katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu.

Yesu daima anaendelea kufanya hija na waja wake katika maisha yao ya kiimani, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashirikisha jirani zao ile furaha ya kukutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha. Waamini wawe wadumifu katika maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; tayari kumwachia nafasi ili kuwafunda kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo; tayari kuondokana na ubinafsi pamoja na kukumbatia malimwengu.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwataka waamini kujenga utamaduni wa kutoka, tayari kuwatangazia jirani zao Injili ya matumaini; kwa kujenga Kanisa linalojikita katika mshikamano wa umoja, udugu na upendo, ili kushirikishana na wengine katika furaha ambayo Yesu amewakirimia katika mioyo yao!

Kongamano hili limezinduliwa na Askofu Vicente Bokalic Iglic, Mwenyekiti wa Tume ya Utume wa walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, ambaye kwa namna ya pekee kabisa, amefafanua mchango wa shughuli za kimissionari zilizotekelezwa na Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume nchini Argentina. Anawataka waamini walei kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa kutangaza Injili ya furaha kwa watu wa mataifa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Vyama vya kimissionari vimekuwa na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Argentina, licha ya magumu na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo. Vijana wanahamasishwa kuitikia wito wa Kipadre na Maisha ya kitawa, ili kushiriki katika azma ya Uinjilishaji. Utume wa Kanisa unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya waamini, kwa kutambua kwamba, wao pia ni wadau wa Uinjilishaji, kwani maisha ya Yesu mwenyewe yalijikita katika utume uliokuwa unapania utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni.

Katika kongamano hili, mada kuu tatu zimechambuliwa: Utambulisho wa vyama vya kimissionari katika Kanisa linalotoka ili kuinjilisha; mwelekeo wa maisha ya kiroho katika Waraka wa kichungaji Injili ya furaha “Evangelii gaudium” pamoja na umuhimu wa utangazaji wa Habari Njema ya wokovu, “Ad gentes”. Kongamano hili limetajirishwa na shuhuda za kimissionari kutoka kwa wadau mbali mbali. Makongamano ya kimissionari hufanyika kila baada ya miaka minne nchini Argentina ili kuimarisha ari na mwamko wa kimissionari miongoni mwa waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.