2015-10-13 15:44:00

Kongamano la Ekaristi na Jubilei ya miaka 200 ya Uhuru wa Argentina, 2016


Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 19 Juni 2016 litaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa sanjari na Jubilee ya miaka mia mbili, tangu Argentina ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wahispania. Maadhimisho haya yatafanyika huko San Miguel de Tucuman, mji ambao kunako tarehe 6 Julai 1816 ukajitangazia uhuru wake. Maaskofu Katoliki Argentina wanasema maadhimisho haya yanakabiliwa na changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kipaumbele cha kwanza ni kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, tayari kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu badala ya mwelekeo wa sasa wa kuendekeza kinzani, misigano na hali ya kutoaminiana. Familia ya Mungu nchini Argentina haina budi kuimarisha utambulisho wa kitaifa unaojikita katika haki, amani, ustawi na mafao ya wengi.

Maadhimisho ya Kongamano la 11 la Ekaristi Kitaifa nchini Argentina ni mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini humo, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani na kuendelea kumwabudu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu; Kristo anayeendelea kuonesha uwepo wake kati ya watu wake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Yesu Kristo Bwana wa historia, tuna haja nawe”. Maaskofu wanasema, Yesu Kristo ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, kielelezo cha umoja kwa Familia ya Mungu nchini Argentina.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linabainisha kwamba, uwepo endelevu wa Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni changamoto kubwa inayoitaka Familia ya Mungu kuangalia historia ya nchi yao kwa imani na matumaini, ili hatimaye, kutambua utambulisho wao na changamoto wanazokabiliana nazo, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya imani, haki na huduma makini kwa wananchi wa Argentina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.