2015-10-13 11:48:00

Kongamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi na dhana ya uhamiaji duniani!


Tume ya Maaskofu wa Jumuiya ya Ulaya, COMECE, tarehe 21 Oktoba 2015 mjini Brussels, itaendesha Kongamano la kimataifa kuhusu mabadilio ya tabianchi, litakaloongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya tabianchi na uhamaji wa watu, changamoto na matumaini”. Mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto kubwa ambazo binadamu anakabiliana nazo kwa nyakati hizi, kutokana na madhara yake ambayo hayachagui wala kubagua.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imonesha kuguswa zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo linachangiwa na wataalam wa kisayansi kwa kushirikishana na sera na mikakati inayofanywa na wanasiasa. Lakini, athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa ni chanzo kikubwa cha watu kuhama au kukimbia kutoka katika maeneo yao, ili kutafuta hifadhi ya maisha. Hii ni kutokana na ukame wa kutisha, athari za mafuriko na ongezeko la joto, mambo ambayo pia yamechangia ongezeko la magonjwa ya milipuko.

COMECE inakiri kwamba, bado kuna mashaka makubwa katika suala zima la mabadiliko ya tabianchi mintarafu utekelezaji wa sheria za kimataifa kama njia ya kudhibiti madhara yake yasienee zaidi. Kongamano hili linapania pamoja na mambo mengine, kusaidia kuangalia changamoto kubwa zinazojitokeza kwenye Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika mchakato wa watu kuhama kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine, wakati mwingine katika mazingira magumu na hatarishi.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa makini kwa kutoa majibu muafaka katika nyanja mbali mbali, bila wanasiasa kujitenga na kuwa mbali kana kwamba, hawahusiki. Kongamano hili litawashirikisha wadau katika sekta ya mabadiliko ya tabianchi na uhamiaji pamoja na kuangalia mchango wa Kanisa katika utekelezaji wa mikakati na sera hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.