2015-10-13 10:07:00

Dumisheni misingi ya haki, amani na usalama wakati wa kupiga kura ya maoni!


Baraza la Maaskofu Katoliki Congo katika Waraka wao wa kichungaji kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanawataka wote kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu wakati watakapokuwa wanapiga kura ya maoni ili kurekebisha Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama ili kutoa mwanya kwa Rais Denis Sassou Nguesso kuweza kuwania tena madaraka katika kipindi cha awamu ya tatu, jambo ambalo linapigwa rufuku kwenye Katiba ya sasa.

Wananchi wa Congo watapiga kura ya maoni hapo tarehe 25 Oktoba 2015 ili kuonesha utashi wao kama wanakubaliana na mabadiliko haya ya Katiba au wanapinga na kutaka Katiba ya sasa iendelee kuheshimiwa. Itakumbukwa kwamba, tarehe 27 Septemba, wananchi wengi wa Congo walijitokeza hadharani kupinga mchakato wa kutaka kurekebisha Katiba ya sasa na kundi jingine ni lile linalounga mkono mabadiliko. Majadiliano yalifanyika katika hali ya utulivu, amani na utu wema wala hakuna jambo lililoharibika!

Hizi ni dalili za ukomavu wa kisiasa unaojikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Machafuko, kinzani na mapigano kiasi cha kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia ni mambo yasiokuwa na tija wala mashiko kwa maendeleo ya nchi. Vijana wawe makini ili wasitumiwe na baadhi ya watu wazima kusababisha machafuko na uvunjifu wa amani.

Kwa kusoma alama za nyakati kutokana na kupanda kwa homa ya kura ya maoni kutokana na hofu. Askofu Daniel Mizonzo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo anawataka wanasiasa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha kwamba, wananchi wanatekeleza haki yao ya kidemokrasia katika mazingira ya amani na utulivu na kamwe wasitishwe wala kunyanyaswa. Heshima na uhuru wa kweli ni msingi wa ukomavu wa kidemokrasia. Vyombo vya ulinzi na usalama vina dhamana ya kuhakikisha kwamba vinadumisha haki na amani, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, mwezi Mei, 2014 wakati wa hija yao ya kitume mjini Vatican, aliwataka Maaskofu kutekeleza dhamana yao ya kichungaji kwa kuendelea kuwa kweli ni sauti ya kinabii, kwa kuthamini maisha ya kijamii, demokrasia ya kweli, kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.