2015-10-12 10:02:00

Wajumbe wa Tume ya kipapa ya ulinzi kwa watoto wamaliza mkutano wao wa mwaka


Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto wadogo, imehitimisha mkutano wake wa mwaka ulioanza hapo tarehe 9 hadi tarehe 11 Oktoba 2015, kwa kushiriki katika Ibada za Misa Takatifu zilizokuwa zinaongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Imekuwa ni fursa kwa wajumbe katika ujumla wao kushirikishana pamoja na kufanya upembuzi yakinifu mintarafu taarifa ya makundi ya wajumbe yaliyoundwa mwezi Februari 2015.

Makundi haya yaliundwa ili kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kushirikiana na Makanisa mahalia kwa ajili ya kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia, vitendo ambavyo vimelichafua Kanisa katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine, Tume hii inatoa mwongozo wa kuwalinda watoto wadogo; mchakato wa uponyaji kwa watu walioathirika na nyanyaso za kijinsia; malezi na majiundo makini kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu, Watawa pamoja na viongozi wa Kanisa katika masuala ya elimu. Tume hii ina dhamana ya kutoa elimu kwa familia na jumuiya za Kikristo, kwa kujikita katika taalimungu na tasaufi; sheria za Kanisa pamoja na sheria za kiraia.

Taarifa ya makundi ya tume hii inaonesha utafiri uliofanywa mintarafu majiundo endelevu ya majandokasisi na wanovisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja takatifu na Utawa ndani ya Kanisa; matumizi ya taarifa za watu wanaotuhumiwa kushiriki katika makosa ya jinai; namna ya kuwasaidia waathirika wa nyanyaso za kijinsia.Tangu kuundwa kwake, Tume hii imepokea mialiko kutoka kwenye Makanisa mahalia na kwamba, wajumbe wake wameshiriki pia katika semina na makongamano mbali mbali yaliyohusiana na ulinzi dhidi ya nyanyaso kwa watoto wadogo. Wajumbe wanaridhishwa na ushiriki wao katika matukio haya na kwamba, mkutano mwingine wa Tume hii unatarajiwa kufanyika Mwezi Februari, 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.