2015-10-12 09:10:00

Uzuri na utakatifu wa maisha ya Ndoa unajikita katika Injili ya Familia!


Mababa wa Sinodi wanalihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linaunganisha na kumwilisha katika vipaumbele vyake: Ukweli kuhusu maisha ya ndoa na familia pamoja na huruma ya Mungu inayoambata toba na wongofu wa ndani. Dhana ya usawa wa kijinsia inachanganya na kuharibu maisha na utume wa ndoa, kwani bwana na bibi wameumbwa ili kusaidiana na kukamilishana katika hija ya maisha. Waamini watambue kwamba, familia ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha furaha ya Mungu kwa binadamu, changamoto ya kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutangaza Injili ya Familia.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma, amekaza kusema kwamba, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia wanaendelea na tafakari zao huku wakiwa wamejikita katika ujasiri na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Idadi kubwa ya Mababa wa Sinodi wamechangia mawazo kuhusu hali halisi ya maisha na utume wa familia sanjari na dhamana ya Kanisa katika kuzisaidia familia kutekeleza dhamana yake barabara.

Mababa wa Sinodi wanasema, Familia ya binadamu ni shule ya ubinadamu, ni Kanisa dogo la nyumbani ni chemchemi ya utu na ubinadamu ni msingi wa maisha ya Kanisa na kisima cha miito na utakatifu wa waamini. Ndiyo maana Kanisa halina budi kukuza na kuendeleza tasaufi ya familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Familia, kwa kujikita katika Sala, tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti, kielelezo cha imani tendaji.

Familia zinahamasishwa kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kujikita katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayowakirimia chakula cha maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto za maisha ya kifamilia, huku wakiwa wamemwambata Kristo Yesu pamoja na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayowakumbusha mapungufu yao ya kibinadamu!

Waamini wapende na kuthamini wito wa maisha ya ndoa, chimbuko la miito mingine yote ndani ya Kanisa. Wanandoa watarajiwa wapewe katekesi na mafundisho ya kutosha, ili waweze kutambua dhamana, wajibu na wito unaowakabili katika maisha ya Ndoa na familia. Wasaidiwe tangu mwanzo na kusindikizwa na Mama Kanisa katika hatua mbali mbali za maisha. Hapa Kanisa halina budi kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Familia. Wakati wa shida na magumu, ukweli, haki, huruma na mapendo yapewe kipaumbele cha pekee na kutambua kwamba, Kanisa linapaswa kuonesha ukarimu na msamaha kwa wale wote wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani.

Waamini wafahamu kwa kina na mapana kuhusu Sakramenti ya Ndoa kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na watetezi wa zawadi hii kutoka kwa Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.