2015-10-12 15:31:00

Utume wa familia na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo!


Sehemu ya tatu ya Hati ya kutendea kazi ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inajikita katika utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo, mada inayochambuliwa na Mababa wa Sinodi kwa wakati huu. Kuhusu wanandoa waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena; mchakato wa kuwasaidia wanandoa kama hawa kupokea Ekaristi Takatifu; umuhimu wa kulinda na kudumisha mafundisho na Mapokeo ya Kanisa; haki na huruma ya Mungu; ni kati ya mada zilizopewa uzito wa juu na Mababa wa Sinodi, bila kusahau mchakato wa kubatilisha ndoa zenye utata kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake binafsi “Mitis Iudex”. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa umakini mkubwa.

Hija ya toba na wongofu wa ndani ni muhimu sana kwa wanandoa waliotalakiana na hatimaye, kuoa au kuolewa wanaotaka kupokea Ekaristi Takatifu. Hapa Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kuwa na msimamo mmoja kwa kuzingatia kwamba, Sakramenti ya Ndoa inaweka madhubuti fungamano la kudumu na la pekee kati ya wanaharusi.

Baadhi ya Mababa wa Sinodi wamegusia kuhusu ugumu wa utekelezaji wa mchakato wa kubatilisha ndoa kama ulivyoelezewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Mitis Iudex”, kwani suala hili linagusa kwa undani Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na neema na baraka inayotolewa na Sakramenti hii kwa wanandoa. Baada ya tafakari ya kina, Mababa wa Sinodi wamekumbushwa kwamba, mchakato huu unalenga kuwasaidia wale walioanguka kusimama tena, kwa kutambua kwamba, mwamini kama binadamu anamwelekeo wa kuogelea katika dhambi; ndiyo maana waamini wanaalikwa kukimbilia huruma ya Mungu.

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha sana ili kufunga na kuganga madonda ya dhambi za mwanadamu. Kumbe, Mafundisho tanzu ya Kanisa yanakwenda sanjari na hali halisi, vingine taalimungu itakabaki inaelea katika ombwe na hivyo kuwa ni kikwazo kwa waamini kuambata imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa halina budi kuwasindikiza wanandoa hatua kwa hatua na kwamba, Kanisa lipo kwa ajili ya huduma kwa familia na kamwe wasiwepo waamini wanaotengwa na huruma na upendo wa Mungu.

Kuna uhusiano makini kati ya Mafundisho tanzu ya Kanisa na huruma ya Mungu kama anavyosema Mtakatifu Paulo “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo”  1 Wakor. 6: 12. Hapa waamini wanahimizwa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, kwa kutafuta mafao ya wengi na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao. Ili kudumisha mafungano ya maisha ya ndoa, kuna haja kwa wanandoa watarajiwa kuwa na maandalizi ya kutosha na ya muda mrefu, yatakayofanywa hatua kwa hatua, ili kuwasaidia wanandoa watarajiwa kufikia ukomavu.

Lengo ni kuwawezesha wanandoa watarajiwa kutambua kwamba, Injili ya familia si wazo la kufikirika, mzigo mzito, bali ni kielelezo cha mpango wa Mungu ambao wanapaswa kuuambata, kwani ni chemchemi ya utakatifu wa maisha na msingi thabiti katika maisha ya kifamilia. Mababa wa Sinodi wanawahamasisha vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuambata Sakramenti ya Ndoa, ili hatimaye, kufaidika na neema zinazotolewa na Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa kwa kushuhudia uzuri wa maisha ya Ndoa unaojikita katika Injili ya Familia.

Mababa wa Sinodi wamekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa wanandoa kukumbatia Injili ya Uhai kwa kuthamini zawadi ya maisha, kama anavyofundisha Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kitume “Humanae Vitae” “Uhai wa binadamu”. Wanandoa watambue wajibu wao na kwamba, wanapaswa kuzingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili, kama Kanisa linavyofundisha na kuhimiza, ili wanandoa waweze kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana.

Mahusiano kati ya wazazi na walezi yamepewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Sinodi, kwa kuwataka wazazi hasa upande wa kiume, kutekeleza wajibu wao barabara katika malezi na makuzi ya watoto wao. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watoto wengi wanaopata malezi tenge kutoka kwa mzazi mmoja. Wazazi wajitahidi kuwalea na kuwatunza watoto wao katika ujumla wao. Lakini, ukweli wa mambo unaonesha kwamba, kuna utengano mkubwa unaoneshwa ndani ya familia kiasi hata kinaligusa Kanisa lenyewe. Wanandoa kwa kushirikiana na Mama Kanisa hawana budi kuonesha uaminifu, kwa kuwakumbatia na kuwasaidia wanandoa waliojeruhiwa katika hija ya maisha yao ya ndoa.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kuhimiza mahusiano bora kati ya familia na Wakleri, kwa kuwajengea wachungaji uwezo wa kuwasindikiza wanafamilia kama wachungaji wema. Wawe ni viongozi wanaoonesha wema na ukarimu; huduma na mshikamano, kwa kuthamini ekolojia ya umoja, ambayo wakati mwingine, inaweza kuonesha upendeleo kwa baadhi ya watu. Wanandoa wawe na uwiano bora kati ya kazi na familia; kwa kujitahidi kushiriki kikamilifu katika maisha ya kiroho na kiutu, hususan Jumapili, inayopaswa kuwa ni Siku kuu ya familia.

Hapa Mababa wa Sinodi wamegusia pia ukosefu wa fursa za ajira na athari zake katika ustawi na maendeleo ya familia. Mwishoni, Mababa wa Sinodi wanasema, familia hazina budi kushirikiana na taasisi na kwamba, Kanisa linahamasishwa kuhakikisha kwamba, linashikiri kikamilifu katika maisha ya hadhara, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwegu. Taasisi na familia zishirikiane kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu.  

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.