2015-10-12 08:04:00

Angalieni mali na utajiri visiwe vikwazo katika hija ya imani!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 11 Oktoba 2015 amesema kwamba, imani na kukumbatia utajiri na mali ni mambo ambayo hayaendi pamoja. Lakini,  mwamini anayejiaminisha kwa Yesu, huyo ana uhakika wa furaha na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu amechambua kwa kina mahojiano yaliyofanywa kati ya Yesu na kijana tajiri aliyempigia magoti akitaka ampatie ushauri ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu baada ya kuwa amezishika amri za Mungu tangu akiwa mdogo. Baba Mtakatifu anasema, Mwinjili Marko katika tukio hili anawazamisha wasikilizaji wake katika mambo makuu matatu ambayo Yesu anayaangalia kwa jicho la pekee kabisa.

Tukio la kwanza ni kijana tajiri kumkimbilia Yesu, ili aweze kupata uzima wa milele, yaani furaha isiyokuwa na mwisho. Hapa Yesu anatoa muhtasari wa Amri za Mungu unaohitimishwa kwa upendo kwa jirani. Yesu anamwangalia kwa upole na kumpenda yule kijana na kisha anamwambia  kwenda kuuza mali yake yote na kuwagawia maskini na hapo atapata maisha ya uzima wa milele. Mwaliko huu, ulimwacha hoi yule kijana, kiasi cha kutumbukia katika mahangaiko ya ndani, kwani alikuwa amejikita mno kwenye utajiri, kiasi cha kushindwa kutekeleza ile kiu ya furaha ya uzima wa milele.

Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu, jicho la upendo wa Yesu halikugusa undani wa maisha ya yule kijana, kwani moyo wake ulikuwa umegawanyika mara mbili: alikuwa anataka kumpenda Mungu pamoja na kukumbatia mali na utajiri. Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani kamwe haiwezi kuambata uchu wa mali na utajiri, daima vitasigana tu. Kijana hakuweza kukubali mwaliko wa Yesu na kufanya mabadiliko, hii ni changamoto kwa waamini kukubali mwaliko wa Yesu unaowaokoa kutoka katika uchu wa mali na utajiri katika hali ya unyenyekevu, tayari kukumbatia upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu.

Waamini wanaalikwa kutokutumbukia katika ndoto zinazowadanganya kwa kupenda mno: fedha, anasa na mafanikio ya haraka haraka, ambayo mara nyingi yanawadanganya na kuwaacha wakiwa wakavu, huku wakielea katika ombwe! Yesu anawataka wafuasi wake kujikita katika maisha ya kweli yanayoongozwa na mwanga angavu!

Baada ya Mitume wa Yesu kusikiliza kwa makini majibu yaliyotolewa na Yesu, wakashikwa na bumbuwazi, akawakazia macho kwa kusema kwamba, ni vigumu kwa matajiri kuweza kuingia katika Ufalme wa Mungu. Lakini, Yesu anawatia moyo kwa kuwaangalia kwa jicho la upendo kwamba, yale yasiyowezekana kwa binadamu, kwa Mungu yanawezekana. Maisha ya uzima wa milele yanaweza kushindikana kwa binadamu, lakini kwa Mwenyezi Mungu ni sawa na maji kwa glasi! Jambo la msingi ni kwa waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kushinda na kuvuka vikwazo vyote vinavyoweza kukwamisha mchakato wa kumfuasa Yesu kwa ukamilifu na uhuru kamili. Waamini washinde vikwazo vya imani wanavyoweza kukutana navyo katika hija ya imani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema kwamba, wale wote walioacha yote kwa ajili ya Yesu na Injili watapata maradufu hapa duniani pamoja na udhia. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuwa huru ili waweze kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani; waache yote ili waweze kupata furaha ya uzima wa milele. Papa amewaambia vijana waliokuwa wanahudhuria sala ya mchana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, waambatane na Yesu, ili aweze kuwakirimia maisha ya uzima wa milele na kamwe wasikubali kufumbata mambo ya dunia yatakayowaacha wakiwa na huzuni moyoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.