Mwishoni mwa wiki ya kwanza ya Mkutano wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu juu ya familia iliyoanza rasmi Jumatatu 4 Oktoba 2015 mjini Vatican, Jumamosi baada ya kukamilisha kazi za mikutano,ikiwa ni siku ya sita, Padre Thomas Rosica CSB, Afisa Mwambata wa Vyombo vya habari vya Jimbo la Papa, aliungana na Padre Federico Lombardi SJ, Mkuu wa Idara ya Habari Vatican, kutoa muhtasari wa majadiliano ya Sinodi kwa waandishi wa habari.
Padre Lombardi, akilenga katika kazi za sinodi kwa siku mbili za mwisho yaani Ijumaa na Jumamosi aliwaambia wanahabari kwamba, masuala kadhaa yameshughulikiwa kupitia majadiliano ya vikundi vidogovidogo vya Mababa wa sinodi, huku wakiendelea na kutoa michango yao juu ya sehemu ya pili ya rasimu ya kufanyia kazi shughuli zao (Instrumentum Laboris). Na mara walipokamilisha sehimu hiyo ya pili, walianza pia kusikiliza michango ya wajumbe kwa ajili ya sehemu ya tatu ya rasimu.
Padre Lombardi aliendelea kutaja, katika kipindi hiki, jumla ya michango 75 imetolewa
katika vikao vya pamoja kutoka Mababa wa Sinodi wakiwakilisha maeneo ya Ulaya, Afrika,
Mashariki ya Kati, na Amerika ya Kusini. Na kulikuwa pia na michango michache kutoka
eneo la Amerika ya Kaskazini.
Na kati ya mandhari zilizoibuka katika michango hiyo ni pamoja na hali ya kiroho ya
maisha ya familia, wajibu wa kimisionari kwa familia katika kutunza na kuendeleza
ndoa bora, uwajibikaji katika majukumu na harakati mbalimbali za familia katika Kanisa,
na kwa jinsi gani Kanisa linaweza kubaki karibu na kutoa msaada kwa familia zinazokabiliwa
na matatizo katika yote kiroho na kihali pia.
Pia kulikuwa na michango kadhaa juu ya uhusiano na uwiano kati ya haki na msaada.
Na kwamba katika mada hii kulikuwa na maoni tofauti tofauti juu ya suala hili miongoni
mwa Mababa. Mmoja wa Baba alisema kuwa huruma haimaanishi kutelekeza mafundisho ya
Kanisa.
Katika Mkutano huu wa wanahabari, Mgeni rasmi alikuwa Mwenye Heri Baselios Cleemis
Thottunkal, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India, ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa
Katoliki katika eneo ya Syro- Malankara. Naye aliwaambia wanahabari kwamba, huruma
maana yake ni kukubali kubadiliko ya kiroho pande zote mbili. Injili inataka hilo
kutendeka kama sharti kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia,ongokeni, alisema.
Aidha Mababa wa Sinodi walionyesha kujali hali ya familia za wanajeshi, ambao kwa mara nyingi hufanya kazi zao za kijeshi mbali na nyumbani kwao mbali na familia zao tena inaweza kuwa kwa kipindi kirefu. Hawa wanaume na wanawake, kama inavyotakiwa kwa familia zao, pia wao wanajeshi wana haja ya kupata huduma maalum kichungaji.
Pia Mababa wa Sinodi, wameonyesha kukubali kwamba, kutokana na hali tofauti na
mazingira tofauti, haiwezekani kuwa na mlingano wa familia au kama "familia ya kawaida".
Wajumbe wengi walizungumzia jinsi isivyokuwa rahisi kwa waliopokea sakramenti ya ndoa
kutangua ndoa, maana huo ni utambulisho muhimu wa ndoa ya Kikristo.
Michango mingi ya Mababa wengi wa Sinodi, ilizungumzia kwa kina, umuhimu wa kuwa na
maandalizi thabiti kwa wachumba wanaotaka kufunga ndoa kanisa. Wametaja kuwa, ni muhimu
sana kwa wachumba kupata majiundo na malezi ya kutosha kabla ya ndoa, ili wapate
ufahamu kamili wa kile wanachotaka kukifanya, kwamba mara wakisha kula kiapo altareni
hakuna tena namna ya kutangua maamuzi yao. Mababa wa Sinodi waliona tatizo hasa kwa
wanaotaka kutangua ndoa, ni ukosefu wa umakini wa kutambua wanachokifanya tangu mwanzo
wa uchumba. Mjumbe mmoja alisema kuwa, Maaskofu wenyewe wanapaswa kukubali kosa lao
kwamba, wameshindwa kutoa malezi ya kutosha kwa waumini wa kawaida katika suala
hili. Na mchango mwingine ulishauri kwamba, wachumba kama ilivyo katika malezi ya
au maisha ya kitawa ni lazima wapitie kipindi cha "Unovisi” kabla ya kuingia katika
sakramenti ya ndoa. Kulikuwa na fikira kwamba, vipeo vinavyoonekana katika miito
ya Upadre na Utawa, pia ni mgogoro huohuo unaoonekana katika maisha ya ndoa na familia.
Pia Wanahabari waliuliza maswali mbalimbali kuhusu mchakato wa Sinodi, kufuatia pendekezo lililotolewa kwamba, kwa siku zijazo , inafaa mchakato ufanyike kwanza katika katika ngazi ya bara, na kisha maoni ya bara yafikishwe katika Mkutano Mkuu wa Sinodi ya kawaida kwa uchambuzi wa mwisho. Hii ina maana kwamba masuala yatakuwa yamejadiliwa kwa umakini zaidi na kuandaliwa vyema, kulingana na mazingira ya bara, kabla ya kufikishwa katika Mkutano wa Sinodi ya jumla ya Kanisa la Ulimwengu . Mwenye Heri Kardinali Thottunkal alijibu hoja hiyo,kwa kuonyesha kukubaliana na hoja akisema, ni kweli inafaa hoja kuanza kujadiliwa katika mazingira ya ndani ya nchi na bara, kabla ya kuletwa katika Mkutano wa Sinodi kama huu. Na kwake yeye, hakuna utata katika mfumo wa mbinu hii na wazo kwamba, mchakato kama huo unaweza kuwa na matunda bora zaidi kwa ajili ya kanisa zima.
Padre Federico Lombardi , alifafanua kwamba, Rasimu ya kufanyia kazi (Instrumentum Laboris) inaweza kubadilishwa iwapo maoni ya wajumbe wengi katika makundi madogomadogo ya vikao vya Sinodi , wengi watapendekeza mabadiliko. Pendekezo kisha, litafikishwa katika Kamati ya Sinodi. Na aliwakumbusha wanahabari kwamba, michango inayotolewa na wajumbe katika vikao si mapendekezo kwa Sinodi; lakini ni sehemu ya "mazungumzo" tu ya Mkutano wa Sinodi.
Aidha Padre Federico Lombardi alisema , athari za uhamiaji, ni hoja iliyokuwa ikijirudia
mara kwa mara katika majadiliano ya Sinodi katika wiki ya kwanza. Kardinali Thottunkal
alisema kuwa yeye anakubaliana na wazo la Papa Francisco, linalo himiza watu wote
kuwapokea wahamiaji katika misingi ya Msamaria mwema. Lakini hata hivyo akasema, alipenda
kuongeza maoni yake binafsi katika hilo, akionyesha imani yake kwamba, jumuiya ya
kimataifa na viongozi wa nchi na serikali, wanapaswa kufanikisha kila linalowezekana
kwa watu kubaki katika nchi zao . Na kwamba ni lazima kufanya kila jitihada za kuhakikisha
watu wanabaki nchini mwao, alisema.
Mababa wa Sinodi, baada ya mapumziko ya Jumapili, wataanza tena kazi zao siku ya
Jumatatu asubuhi.
All the contents on this site are copyrighted ©. |